Rais Samia aagiza mchakato wa ajira 6,000 za walimu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora kuajiri walimu 6,000 haraka.kuangalia nafasi za ajira za walimu takribani 6,000 na kutangazwa haraka,anaripoti Fred Kibano (Dar es Salaam).
Agizo hilo amelitoa Ikulu ndogo Jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha Makatibu wakuu wa Wizara, Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara na Wakuu wa Taasisi na Idara mbalimbali za serikali hii ambapo ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora kuajiri walimu wapya 6,000 wanaotokana na walimu walioacha kazi, kufariki na kustaafu ili kuziba pengo la watumishi hao kwenye sekta ya elimu nchini.

Akitoa hotuba yake iliyojaa maagizo ya Serikali kwa viongozi wateule, Mhe. Samia Suluhu Hassan amemwagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Ummy Mwalimu kuendelea na ujenzi wa miundombinu ya sekta ya Afya na Elimu inayoendelea kujengwa ili ikamilike kwa wakati na wananchi wengi wanufaike na huduma za elimu na huduma za afya. 

Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza Ofisi ya Rais TAMISEMI kuendelee na ujenzi wa shule 26 zinazoendelea kujengwa kila mkoa ambazo bajeti yake ipo tayari na kwamba zikamilike kwa wakati na kuanza kazi.  

Kwenye sekta ya afya, ameagiza kuendelea kwa ujenzi wa hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati lakini pia kuhakikisha vituo vya afya vilivyokamilika vimewekewa dawa na vifaa tiba ili vianze kutoa huduma mara moja na kuondoa kero kwa wananchi.

Agizo jingine ni kuona namna ya kutoa ajira mpya za madaktari kwenye vituo vipya vya afya na hospitali za wilaya nchini ambazo zinatokana na uhaba wa wataalam hao kutokana na kukamilika kwa miundombinu mingi ya afya kwenye Mikoa na Halmashauri pamoja na kuwa bajeti ya mwaka huu ni kuongeza vifaa tiba na dawa. 

Kuhusu Wakala wa barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kuangalie njia ya kufanya kwa pamoja ili kutengeneza barabara za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa fedha za Halmashauri husika kama zipo na kwamba fedha zitakazotoka hazina kwa ajili ya barabara zipelekwe kwenye barabara nyingine kwenye Halmashauri husika.

Katika Hatua nyingine, Rais Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa Mikoa na Halmashauri kuacha kuwazuia watu kuandika kero zao kuhusu mambo yanayowasibu kwa kuwaficha baada ya kuandika kwenye mabango kwani njia pekee ni kutatua kero zinazowakabili wananchi.

Vilevile, amewataka viongozi na watendaji kusimamia makusanyo ya mapato na matumizi yake kwa kutumia kanuni na sheria bila kuwa kera kwa wafanyabiashara. 

Mwisho ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI kuongeza nguvu kwenye usimamizi wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kazi ifanyike kwa ufanisi na kuwa na matokeo chanya lakini pia amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa bidii na kuwatumikia watanzania bila upendeleo.

Post a Comment

0 Comments