Rais Samia, Dkt. Mwinyi waonyesha misimamo kuwatumikia Watanzania bila ubaguzi

Samia Suluhu Hassan ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewaonya wabunge ambao amesema wanajikita kumlinganisha yeye na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli huku akiwataka kufanya kazi za kibunge ikiwemo kujadili bajeti za wizara mbalimbali na si vinginevyo, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.

Mheshimiwa Samia ameyasema hayo leo Aprili 18,2021 baada ya kuwaongoza viongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Kongamano la viongozi wa dini nchini wakiliombea Taifa na kumshukuru Mungu kwa maisha ya Hayati Dkt.John Pombe Joseph Magufuli ambalo limefanyika kwenye Ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma.

“Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nawashukuru viongozi wa Dini kwa kongamano hili na asante kwa kutupa mwaliko viongozi, natambua mchango mkubwa wa Hayati Magufuli kwa jinsi alivyowathamini na mimi pamoja na Dkt. Mwinyi tutaendeleza utamaduni huo. Inasikitisha kuona kwamba watu wanapiga ngoma mitandaoni, lakini inachezwa Bungeni, mnamlinganisha Magufuli na Samia, hawa watu ni kitu kimoja, nafuatilia mijadala yenu bungeni haina afya kwa Taifa, mjikite na upitishaji wa bajeti.
"Awamu ya Sita haikutokana na uchaguzi, haikutokana na chama kingine cha siasa, imetokana na CCM, awamu ni maneno tu ila mambo ni yaleyale, mwelekeo wa Awamu ya Sita ni kudumisha mema yaliyopita,kuendeleza mema yaliyopo na kuleta mema mapya ndio maana ya kazi iendelee, kazi imeshafanywa tunaiendeleza,”amefafanua Rais Samia.

Rais Samia amesema kuwa, ndiyo maana hata alipounda Baraza la Mawaziri, alifanya maboresho ya kuwahamisha baadhi lengo likiwa ni kuboresha na ataendelea kufanya hivyo.

"Tukumbuke tupo kwenye Mwezi wa Toba (Ramadhan), naomba muendelee kuliombea Taifa letu, Nchi yetu haina Dini lakini Katiba ya Nchi yetu imetoa uhuru kwa Wananchi kuabudu Dini wanazotaka na hii imefanya kuwe na ushirikiano mkubwa, sio kila Nchi jambo hili linawezekana. Viongozi wa Dini mkiongea yanabaki kwenye mioyo ya Watu, Sisi Viongozi wa Siasa tukiongea yanabaki kwenye vichwa vya Watu, vichwa vikichanganywa na mambo mengi yanatoka na huu ndio umuhimu wa Viongozi wa Dini kufanya kazi na Sisi, mtatusaidia kusema tunayotaka kusema,"amefafanua Rais Samia.

Naye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa maisha ya Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli yalikuwa ni darasa tosha kwa viongozi na Watanzania wote juu ya namna wanavyotakiwa kuishi.

Rais Dkt. Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo katika salamu zake alizozitoa huko katika ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma katika Kongamano la kumuombea dua Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ambalo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi.

Katika salamu hizo, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, Rais Magufuli alikuwa kiongozi mwenye kumtegemea sana Mwenyezi Mungu na kuamini kuwa yeye ndiye Muweza wa kila jambo.

Amesema kuwa, Hayati Magufuli alipigania umoja na alikuwa karibu sana na viongozi na waumini wa dini na madhehebu yote na kila mara aliwataka waumini wa dini zote kuiombe nchi na pia, hakusita kusaidia maendeleo ya dini bila ya ubaguzi.

Amesema kuwa, imani yake hiyo ilimfanya ajiamini na kuwa na uthubutu wa kuchukua maamuzi mazito kwa yale aliyoamini na yenye manufaa kwa wananchi wa Jamhuri ya Muuugano wa Tanzania.

Ameeleza kuwa Marehemu kila mara alikuwa akihimiza kufanyakazi kwa bidii kwa kutumia wito wake wa “ Hapa Kazi tu” na maneno aliyoyatohoa kutoka kwenye vitabu vya vitakatifu yasemayo “ Asiyefanya kazi asile” maneno ambayo yatakumbukwa kama dira ya uwajibikaji

Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Hayati Magufuli aliwafunza Watanzania kuwafikiria zaidi wanyonge na watu wenye mahitaji maalum mambo ambayo alitekeleza kwa vitendo ikiwemo kutoa elimu bure, ujenzi wa hospitali za kisasa, kuweka mkazo juu ya usambazaji wa huduma za maji, umeme vijijini, ujenzi wa miundombinu ya barabara pamoja na kushughulikia kero za wafanyabiashara wadogo wadogo.

Katika salamu zake hizo, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa Hayati Magufuli hakuwa na kigugumizi katika kukemea na kupiga vita vitendo vya rushwa, wizi, uzembe na ubadhirifu wa mali ya umma ambapo ameacha mfano katika usimamizi wa matumizi bora ya fedha na rasilimali za taifa.

Rais Dkt. Mwinyi alisema kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina upekee wa kuwa na rasilimali mbali mbali na kuwa ni mfano Barani Afrika na duniani kote katika kudumisha amani, umoja na mshikamano.

Alisema kuwa Tanzania inaendelea kuonesha ukomavu katika kudumisha demokrasia na utawala bora ambapo Tanzania ina utaratibu mzuri wa Kikatiba wa kubadilisha uongozi hata pale ambapo Mwenyezi Mungu analeta mtihani wa kuomdokewa na viongozi wa Kitaifa, Tanzania huwa inafuvu.

Aliongeza kuwa hivi sasa Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa duniani kwa kuwa na Rais mpya ambaye ni Samia Suluhu Hassan ambae ni Mama wa kwanza kushika nafasi hiyo kubwa hapa nchini na pia katika eneo la Afrika Mashariki.

Aidha, alisema kuwa Rais Samia ana mchango mkubwa katika kuiongoza Tanzania kufikia maono ya Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Magufuli sambamba na kuendeleza fira zake.

Kwa msingi huo, Rais Dk. Mwinyi aliwaomba Watanzania kumpa mashirikiano ya kutosha ili aendelee kusimamia kazi iliyoanzishwa na Hayati Rais Magifuli.

Rais Dk. Mwinyi aliahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itampa ushirikiano wa kutosha Rais Samia katika kufanikisha majukumu yake.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Miwnyia lsiema kuwa anaungana na viongozi wa dini katika kumuombea dua Hayati Magufuli pamoja na nchi kwa ujumla.

Wakati huo huo, Askofu wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Peter Konki alisema kuwa, wanasiasa wanapaswa kuacha kujipendekeza kwa Rais Samia ili waweze kuteuliwa katika nafasi mbalimbali.

"Nimeona kwenye mitandao ya kijamii wanasiasa wakimsifia Rais Samia na kumkashifu Hayati Magufuli, hii ni kujipendekeza ili wateuliwe kwenye nafasi mbalimbali, huu ni unafiki mkubwa sana, Hayati magufuli ni kipenzi cha wengi, hivyo wanasiasa wasitugawanye,"Alisema Askofu Konki.

Post a Comment

0 Comments