Serikali ya Tanzania yasitisha bei mpya za vifurushi vya (data) intaneti

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo ni Mdhibiti wa Sekta ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta nchini imesitisha kwa muda matumizi ya bei mpya ya vifurushi vya data ili kutoa nafasi kwa watoa huduma kupanga upya bei za vifurushi kwa ufanisi na kufanya uchambuzi wa kina kwa ajili ya kulinda maslahi ya watumiaji,anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Dar es Salaam).
Picha na information-age

Hayo yamebainishwa leo Aprili 2, 2021kupitia taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandishi James M. Kilaba.

Amesema, pamoja na mambo mengine, TCRA ina jukumu la kusimamia gharama na tozo katika huduma za mawasiliano zinazotolewa na Watoa huduma na kuwalinda watumiaji wa huduma hizo.

"Mnamo tarehe 5 Februari, 2021, TCRA ilitoa tangazo la kukaribisha maoni ya wadau kuhusu huduma za vifurushi zinazotolewana Watoa huduma za mawasiliano ya simu za mikononi. Kutokana na maoni hayo, TCRA iliandaa Kanuni ndogo za Vifurushi (Rules)za mwaka 2021,zenye lengo la kuweka utaratibu kwa Watoa huduma wa namna ya kupanga vifurushi, bei na muda wa matumizi ya vifurushi hivyo.

"Kanuni hizo zimeanza kutumika tarehe 02 Aprili, 2021.Katika utekelezaji wa Kanuni hizi, watoa huduma waliwasilisha idadi na bei ya vifurushi vipya pamoja na bei za huduma nje ya vifurushi. TCRA imeidhinisha idadi ya vifurushi vilivyowasilishwa pamoja na bei za huduma nje ya vifurushi na tayari zimeanza kutumika tarehe 02 Aprili 2021.

"Hata hivyo, TCRA imesitisha kwa muda matumizi ya bei mpya ya vifurushi vya data ili kutoa nafasi kwa Watoa huduma kupanga upya bei za vifurushi kwa ufanisi na kufanya uchambuzi wa kinakwa ajili ya kulinda maslahi ya watumiaji.TCRA itaendelea kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu huduma za mawasiliano kwa ustawi na maendeleo ya Taifa,"ameeleza Mhandisi James M. Kilaba kupitia taarifa iliyoonwa na DIRAMAKINI.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news