Serikali yabaini hujuma katika vifungashio na mifuko

Operesheni maalum ya kusaka vifungashio na mifuko iliyo chini ya kiwango imebaini ujanja unaotumika na wazalishaji kwa kuchanganya katikati vifungashio vyenye ubora na visivyo na ubora kwa kuhofia kukamatwa,anaripoti Pamela Mollel.
Akizungumza jijini Arusha,Mkaguzi wa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la hifadhi ya mazingira Kanda ya kaskazini Justine Kasoka alisema kuwa katika oparesheni hiyo wamebaini udanganyifu unaofanywa na wazalishaji wa vifungashio hivyo kwa kuchanganya na visivyokuwa na ubora.

Ameongeza kuwa, wazalishaji wanachanganya vifungashio vyenye nembo na taarifa zinazotoa maelezo na vile ambavyo havina kabisa yaarifa yoyote sehemu vinapotoka jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Pia ametoa rai kwa makampuni na viwanda vinavyozalisha mifuko mbadala kuhakikisha wanazingatia sheria inavyowaelekeza kwa kuweka chapa pamoja na maelekezo yote yanazingatiwa kwa kuwa zoezi la ukamataji limeanza rasmi na yule asiyezingatia maelekezo hatua Kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Amesema, mifuko yote mbadala isiyokuwa na nembo na taarifa kamili inapotoka pamoja na nembo ya Shirika la Viwango Nchini ( TBS) ikiwa ni pamoja na mifuko laini isiyokidhi viwango hairuhusiwi na tayari zoezi la ukamataji limeanza kwa wafanyabiashara wanaokiuka taratibu na sheria ya mazingira.

Amewapongeza wananchi wa jiji la Arusha kwa kutokomeza mifuko hiyo kwa kiwango kikubwa huku akisema katika zoezi hilo wamebaini kuwa wafanyabiashara wadogo wadogo waliowengi hawakukutwa na vifungashio vilivyochini ya kiwango isipokuwa wachache walionunua bila kugundua kuwa ndani vimechanganyikana na visivyohitajika .

Naye mfanyabiashara wa viungo soko la Kilombero, Celina Fredy aliiomba Serikali iwakumbuke walaji wachini ili kuwepo na vifungashio vya bei ya chini vinavyoendana na hali yao. Zoezi hilo lilifanyika katika eneo la Soko kuu,Soko la Kilombero na Soko la Samunge

Post a Comment

0 Comments