Serikali yatenga milioni 311.9/- kuchonga barabara hifadhi ya Rumanyika na Ibanda

Serikali imetenga shilingi milioni 311.9 zitakazotumika kuchonga barabara yenye urefu wa kilomita 20 katika hifadhi ya Taifa Rumanyika Karagwe na kilomita 51 katika Hifadhi ya Taifa ya Ibanda Kyerwa katika mwaka wa fedha 2020/2021, ANARIPOTI John Bera (WMU).
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Francis Masanja akijibu swali la Mhe. Innocent Sebba Bilakwate wakati wa mkutano wa 3 Kikao cha 5 cha Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aprili 8, 2021 jijini Dodoma.

Kauli hiyo ilitolewa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, Innocent Sebba Bilakwate (CCM) ambaye alihoji kuhusu mpango wa Serikali wa kuweka miundombinu mizuri ya barabara katika hifadhi hizo Ili kuvutia watalii.

Akijibu Swali hilo kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro, Masanja ameeleza kuwa, hifadhi za Taifa za Ibanda Kyerwa na Rumanyika Karagwe zilianzishwa kupitia tangazo la Serikali Na 509 na 510 la tarehe 5/7/2019 .

Amesema, hifadhi hizo zilitokana na kupandishwa hadhi kwa yaliyokuwa mapori ya akiba ya Ibanda na Rumanyika.

"Ili kuwezesha hifadhi hifadhi hizo kufikika kwa urahisi Serikali kupitia TANROADS na TARURA iliyokuwa ikitengeneza barabara mbalimbali zinazorahisha kufika kwa watalii katika hifadhi hizo, barabara hizo ni pamoja Mgamkorongo iliyopo wilaya ya Korogwe hadi Murongo wilayani Kyerwa yenye urefu wa kilomita 112 ambayo inafanyiwa matengenezo na TANROADS kila mwaka na imewekwa katika mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami katika mwaka wa fedha 2020/2021,"amesisitiza Masanja.

Aidha, amesema jitihada hizo za kuboresha miundombinu ya barabara katika hifadhi ya Taifa Ibanda Kyerwa na Rumanyika Karagwe na maeneo mengine yote ya hifadhi zitasaidia kuweka mazingira mazuri yatakayowezesha hifadhi hizo kutembelewa na watalii wengi wa maeneo ya karibu pamoja na wageni kutoka nchi jirani.

Kuhusu ulinzi wa maeneo hayo ameeleza kuwa wizara imekuwa ikiyaanisha maeneo yote na kuweka mipaka.

"Katika hifadhi ya Ibanda Kyerwa na Rumanyika tulifanya tathmini baada ya wataalamu wetu kuainisha mipaka, utekelezaji wake tunaendelea nao kwa kuandaa Mazingira ya kuwapeleka wataalamu kwa ajili ya gharama za uthamini na kuanisha maeneo ambayo yana changamoto za uhifadhi,"amesisitiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news