TAMISEMI ni kubwa sio ngumu-Waziri Ummy

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Ummy Mwalimu amewataka watendaji wa TAMISEMI kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikano, ubunifu, uzalendo na uadilifu ili kurahisisha utendaji kazi,anaripoti Angela Msimbira (TAMISEMI).
Akiongea leo na Menejimenti ya ofisi hiyo katika hafla fupi ya ukaribisho Mtumba jijini Dodoma, Waziri Ummy amesema kuwa atahakikisha anafanya kazi kwa ushirikiano, umoja na kujituma ili kuhakikisha TAMISEMI inakidhi matarajio ya Rais na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

“Baadhi ya watu wanasema TAMISEMI ni ngumu, mimi nasema TAMISEMI sio ngumu, kama TAMISEMI ni ngumu maana yake mmeshindwa kunisaidia mimi na Manaibu Waziri kutekeleza wajibu wetu, ila tunakubali ni kubwa lakini hakuna kigumu kama kuna utendaji kazi wa pamoja,"amesisitiza Waziri Ummy.
Amefafanua kuwa kinachohitajika ni kufanya kazi kwa umakini, utekelezaji wa majukumu kwa wakati, na kuhakikisha tunaendeleza pale alipoachia aliyekuwa Waziri wa Nchi – TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo.

Aidha, Waziri Ummy amesema vipaumbele atakavyoanza navyo kuvifanyia kazi ni kupitia hoja zilizoibuliwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hasa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizopata hati chafu nane na zenye mashaka 53.

Amesema vingine ni kuimarisha usimamizi wa makusanyo ya ndani na matumizi katika mamlaka hizo, ushirikiano na ubunifu, usimamizi wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo na urejeshaji wa fedha za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kadhalika, amesisitiza kuzitambua changamoto zilizopo sekta ya afya, elimu na miundombinu ili kuzipatia ufumbuzi.

“Mmemsikia Spika(Job Ndugai) hivi Mkurugenzi unakuwaje na amani wakati watoto wanakaa chini, kitu kama madawati hivi Mkurugenzi anajisikiaje watoto kukaa chini, hivi sisi TAMISEMI tunashindwa kuja na mkakati wa kuondoa tatizo la watoto kukaa chini, hivi TAMISEMI tunashindwa kuhakikisha madarasa yanajengwa ili watoto wasirundike kwenye madarasa wa kuwa na madawati na madarasa, nyumba za walimu hiki ni kipaumbele changu,”amesema. Waziri Ummy

Kuhusu utoaji wa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, Waziri Ummy ametaka kujua fedha zilizorejeshwa na kuzitaka Halmashauri kueleza mrejesho ili fedha zitolewe zaidi.

“Sitaki kusema mimi ni hodari bali ni hodari wa kushirikiana na wenzangu naamini tutakwenda vizuri,na kubwa lazima tuonyeshe matokeo hasa kwenye ukusanyaji wa mapato,”amesema.

Aidha amewaagiza Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini(TARURA), kushughulikia hoja zilizobainishwa na wabunge huku akisisitiza suala la uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news