Umoja wa Mataifa wataja mambo yatakayomfanya Hayati Dkt.Magufuli kuendelea kuenziwa

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limemuenzi na kumkumbuka aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania,Hayati Dkt.John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, mwaka huu, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.
Antonio Guterres ambaye ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameyasema katika hotuba yake akimwelezea Hayati Magufuli kuwa alijitahidi kupanua huduma za kijamii na kukabiliana na rushwa nchini Tanzania.

Amesema, Hayati Rais Dkt.Magufuli alichagiza maendeleo ya miundombinu na viwanda ambavyo vitu muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi.

Guterres amesema, chini ya hayati Magufuli Tanzania ilifikia azma ya kuwa nchi ya uchumi wa miaka minne kabla ya lengo lililokuwa limewekwa la mwaka 2025.

Katibu Mkuu pia amegusia elimu akisema kuwa Hayati Magufuli alisaidia kuimarisha mfumo wa elimu na kuongeza viwango vya uandikishaji wa wanafunzi wapya kujiunga na shule za sekondari.

Amesema,serikali yake ya awamu ya tano, iliimarisha usambazaji umeme vijijini ikiwa na lengo la kupanua uwezo wa wananchi kupata umeme nchi nzima.

Kiongozi huyo ametuma kwa mara nyingine salamu za rambirambi kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, kwa wananchi na serikali ya Tanzania Pamoja na familia ya hayati Dkt. Magufuli.

Katibu Mkuu amesema, Umoja wa Mataifa unatambua historia ya muda mrefu ya taifa hilo la Afrika Mashariki katika kusongesha ushirikiano wa kimataifa na amepongeza jinsi inavyojitoa katika ushirikiano huo wa kimataifa na kikanda.

"Natumia fursa hii kusisitiza na kukazia azma ya Umoja wa Mataifa ya kuendelea kushiriana kwa karibu na Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan, rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania. Tuko Pamoja na wananchi wa Tanzania katika kusongesha maendeleo endelevu na kuunga mkono jitihada zake za ustawi wa wananchi wote,"amesema.

Katika kikao hicho, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Profesa Kennedy Gastorn alipata fursa ya kuzungumza ambapo alimwelezea Hayati Dkt. Magufuli kuwa alibaini lengo la kizazi chake na kamwe hakusaliti.

"Upendo wake kwa Mungu na Taifa lake, imani yake kwa watu wake, vilimfanya awe mtu wa kipekee mwenye heshima na Rais wa wanyonge,"amesema.

Profesa Gastorn alienda mbali kusema kuwa, Hayati Magufuli alikuwa mtu aliyevutia watu wengi ulimwenguni kote na alizungumza ukweli kupitia ukweli wa uwajibishaji na wakati huo huo kwa unyenyekevu.

“Miongoni mwa watendaji wenzake alikuwa muwazi na kila wakati alikuwa mchapakazi, mzalendo wa dhati na kiongozi ambaye hakupenda ubinafsi,”amesema Balozi Gastorn.

Amezungumzia jinsi ambavyo Hayati Magufuli alikuwa kiongozi mwenye maono na mwanamajumui aliyeamini kuwa kila mtanzania na kila mwafrika na kila binadamu anastahili kitu bora zaidi.

Mwakilishi huyo wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa amesema Awamu ya Tano baada ya kutamatika Machi 17, mwaka huu wa 2021, ukurasa mpya ulifunguliwa wa Awamu ya Sita Machi 19, 2021 kwa kuapishwa kwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vya ulinzi na usalama.

“Tunajivunia kama taifa na tunashukuru kwamba katika hatamu za uongozi, kwa mara ya kwanza tuna Mwanamke ambaye ni Mkuu, ikiwa ni historia. Rais Samia ni mzalendo na mwanasiasa anayezingatia misingi, ana maono na muumini na muungaji mkono wa ushirikiano wa kimataifa,”amesema.

Hata hivyo, chini ya uongozi wake, Tanzania itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Umoja wa Mataifa na misingi yake ambayo ni amani na usalama duniani, haki za binadamu, maendeleo na ustawi wa binadamu.

“Rais Samia tayari amechukua hatua za kiuongozi kwa unyenyekevu na ubunifu, kasi na upendo katika kufanikisha ajenda 2030 ya maendeleo endelevu,”amesema Profesa Gaston. (UNnews).

Post a Comment

0 Comments