Vigogo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wang'ang'ania nafasi ya juu

Ayoub Lyanga ndani ya dakika ya 21 amewapatia waajiri wake Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara leo ndani ya dimba la Jamhuri jijini Dodoma, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.

Kwa bao hilo la pekee na ushindi huo unaifanya Azam FC chini ya mwalimu George Lwandamina ifikishe alama 50 baada ya kucheza mechi 26 na kurejea nafasi ya pili sasa ikizidiwa alama moja na Yanga SC ambao hata hivyo wana mechi moja mkononi.

Wakati huo huo, KMC imeitandika Gwambina FC 3-0 ni kupitia mabao ya Charles Ilamfya dakika ya 51, Emmanuel Mbuyekure dakika ya 62 na Ally Ramadhani dakika ya 72.
Aidha, kwa ushindi huo, KMC chini ya mwalimu John Simkoko inafikisha alama 39 baada ya kucheza mechi 26 na kusogea nafasi ya tano ikizidiwa alama moja na Biashara United ambayo hata hivyo imecheza mechi moja zaidi.

Wao JKT wanabaki na alama zao 27 za mechi 26 katika nafasi ya 13 na Gwambina inabaki na alama 30 za mechi 24 nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Aprili 15, 2021 Polisi Tanzania imeichapa Namungo FC mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ndani ya dimba la Ushirika mjini Moshi,Kilimanjaro.

Ushindi wa Polisi Tanzania umechagizwa na mabao ya Kassim Haruna dakika ya 7 na Gerald Mathias dakika ya 19, wakati la Namungo FC limefungwa na Freddy Tangalo dakika ya 57.

Pia Ihefu SC imeichapa Mbeya City 1-0, bao pekee la Andrew Simchimba dakika ya 74 Uwanja wa Highland Estate, Ubaruku wilayani Mbarali Mkoa wa Mbeya.

Post a Comment

0 Comments