Viongozi wa umma msitumie nyadhifa zenu kuwanyanyasa walio chini yenu-Othman Masoud

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amewataka watumishi wa serikali kutotumia nyadhifa na madaraka waliyopewa kama fimbo ya kuwaadhibu watumishi walio chini yao, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI.
Mheshimiwa Masoud ameyasema hayo katika Semina ya mafunzo elekezi kwa makatibu wakuu, manaibu wao pamoja na naibu mwanasheria mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo alitoa mada kwa washiriki hao.

Mheshimiwa Othman Masoud alitoa ufafanuzi zaidi na kusema,

"Tukiwekana kazini kwasababu ya udugu, urafiki au itikadi za vyama vyetu basi ni wazi hatutofanikiwa kufanikisha malengo ya serikali." Suala hili ni moja ya changamoto kubwa inazozikabili sekta za umma visiwani Zanzibar.

Mafunzo hayo ya siku mbili yanayolenga kuwaongezea ujuzi na maarifa watendaji wakuu wa SMZ, yanafanyika katika hoteli ya Sea Cliff iliyopo Michungwa miwili wilaya ya Kaskazini 'B' kwenye mkoa wa Kaskazini Unguja.

Katika mada yake aliyoipa jina la ‘Mambo ya Msingi kwa Utumishi wa Umma’ Mheshimiwa Othman amesema tatizo kubwa lililopo ni baadhi ya watumishi wa umma kutokujali wajibu wao, jambo ambalo linapelekea kuzorotesha au kufelisha kabisa shughili za serikali.

Aliongeza kuwa si vyema kwa viongozi katika taasisi kujiona hakuna zaidi yao na kuwadharau wengine kwani jambo hilo huzusha chuki na kupunguza ufanisi kwa watendaji wa chini.

"Kuwa katika wadhifa mkubwa sio kibali cha kuwanyanyasa walio chini yako. Kama mtendaji kakosea aadhibiwe kwa mujibu wa sheria na siyo kwa kumuonea. Tumeshuhudia hapa wapo viongozi wakiondoka katika madaraka watendaji na wananchi wanafurahi sana wengine hata kufikia kufanya sherehe. Sasa tusifike huko, tutengeneze mazingira rafiki ili kuleta ufanisi na urafiki", alisema Mheshimiwa Othman.

Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alisisitiza pia juu ya umuhimu wa kila wizara kuhifadhi kumbukumbu.

"Tujitahidi sana kuhakikisha katika wizara zetu taarifa za umma tunazihifadhi katika ofisi za nyaraka au gazeti la serikali ili kuweza kusaidia katika kumbukumbu zetu na kwa matumizi ya baadae ikiwemo kutatua migogoro na changamoto zinazoweza kujirejea mara kwa mara", aliwaambia washirki wa mafunzo hayo.

Mheshimiwa Othman alimalizia kwa kuwapa nasaha viongozi hao kwa kuwaambia ya kwamba, "Uzuri wa katiba na sheria hautaweza kutusaidia ikiwa watumishi wenyewe hatujaamua kubadili mitazamo yetu kutoka tulipotoka na kuendana na matakwa ya utumishi na kukubali tulipo sasa".

Post a Comment

0 Comments