Viongozi waandamizi mbaroni kwa kutaka kumpindua Mfalme Abdallah II wa Jordan

Viongozi mbalimbali nchini Jordan wamekamatwa kwa tuhuma za kutaka kufanya mapinduzi dhidi ya Serikali ya Kifalme inayoongozwa na Mfalme Abdullah II bin Al-Hussein (Abdallah II).

Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari duniani vimesambaza ukanda wa video ukimuonesha mrithi wa zamani wa kiti cha ufalme wa Jordan, Hamza bin Hussein akisisitiza kuwa amewekwa kwenye kifungo cha nyumbani yeye na walinzi wake.

Runinga ya al Alam nayo iliweka mtandaoni mkanda huo wa video na kuandika kuwa, mrithi huyo wa zamani wa kiti cha ufalme wa Jordan amewalaumu viongozi wa nchi yake kwa kushindwa kuiongoza vizuri Jordan.

Pia amesema anashangaa kuona kuwa ukosoaji mdogo wa siasa za utawala umepelekea awekwe kwenye kifungo cha nyumbani.

Shirika la Habari la FARS limeripoti kuwa, viongozi wasiopungua 20 wa ngazi za juu pamoja na wakuu wa kikabila na watu wa familia ya kifalme wamewekwa chini ya ulinzi kwa kile kilichodaiwa ni tishio la usalama wa Jordan.

Runinga al Jazeera imemnukuu mwanamfalme Hamza akisema kuwa, ametakiwa na mkuu wa jeshi la Jordan asitoke nje na asiwasiliane na watu na wala asionane nao.

Gazeti la Washington Post limenukuu duru za karibu na familia ya kifalme ya Jordan zikikanusha kuhusika mrithi huyo wa zamani wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo katika jaribio la mapinduzi.

Televisheni ya al Mayadeen imeripoti kuwa, viongozi kadhaa wa ngazi za juu wa Jordan wamekamatwa katika kile kilichodaiwa ni kupanga njama za kuupindua utawala wa mfalme Abdullah II.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news