Waandishi waandaa Dkt.Mwinyi Award na Maalim Seif Award Zanzibar

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari Dkt.Mzuri Issa Ally amesema wameamua kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari kivingine kuliko miaka yote iliowahi kupita nyuma, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Zanzibar).
Mwenyekiti huyo ambaye ni Mkurugenzi wa TAMWA-Zanzibar ameyasema hayo wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la kitivo cha idara ya ya mawasiliano ya chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Kilimani mjini Unguja.

Amesema, kwa mwaka huu kamati hiyo wameamua kuja na muonekano mpya na utakua wa kipekee kuliko miaka yote iliopita nyuma kutokana na kuipa umuhimu siku hio adhimu kwa waandishi wa habari ambayo kila mwaka hufanyika mara moja pekee.

Akieleza baadhi ya mikakati waliojiwekea ni pamoja na kuanzishwa kwa tunzo za waandishi wa habari katika makundi matano tofauti.

Wakati akifafanua makundi ya tunzo hizo amesema ni pamoja na tunzo ya uchumi wa buluu ambayo wameamua kuipa jina la Dkt.Mwinyi ‘’Award’’ kundi la pili likiwa ni tunzo ya uandishi wa habari za Serikali ya umoja wa kitaifa ambayo nayo imepewa jina la Maalim Seif ‘’Award’’.

Aidha, Mkurugenzi huyo amendelea kutaja makundi mengine ambayo ni uandishi wa habari za jinsia ambayo imepewa jina la Mariam Mwinyi ‘’Award’’ na nyingine tunzo ya masuala ya kodi ambayo imepewa jina la ZRB ‘’Award’’huku tunzo nyingine ikilenga masuala ya rushwa na uwajibikaji ambayo imepewa jina la ZAECA ‘’Award’’

Akifafanua zaidi amesema mashindano hayo kwa waandishi wa habari yatazingatia kazi zote zilizotolewa kwenye vyombo vya habari kuanzia mwezi Januari mwaka huu hadi mwishoni mwa mwezi wanne mwaka huu.

Amesema uwepo wa tunzo hizo ni muhimu mno pia itasaidia na kuongeza uwajibikaji Serikalini kwa kuwa tunzo hizo zimezingatia mambo muhimu yanayomgusa kila mtu.

‘’Mashindano haya hayatamalizia hapa na tunaamini pia yatakuza vipaji vya waandishi wetu hapa Zanzibar na itawafanya waweze kujituma zaidi,"ameongeza.

Awali Mwenyekiti wa kamati hio mwandishi wa habari mwandamizi wa ITV, Farouk Kareem aliwataka waandishi wa habari kujitokeza kwa wingi kuwania tunzo hizo ambazo ni mara ya kwanza kutolewa visiwani hapa.

Alisema licha ya uwepo wa tunzo hizo lakini pia kutakua na bonanza maalumu la michezo kwa waadishi wa ahari litakalolenga kuhamaisha ufanyaji wa mazoezi kwa wanahabari visiwani hapa.

Maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari ulimwenguni hufanyika kila ifikapo tarehe 3 ya mwezi wa tano ya kila mwaka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news