Wanaume mnaonyanyaswa katika familia zenu njooni mpate msaada-Polisi

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewataka wanaume wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika familia zao wajitokeze na kudai haki zao mbele ya sheria, badala ya kuendelea kukaa kimya kwa kilea kinachodaiwa wanaona aibu huku wakizidi kuteseka, anaripoti Mwandishi DIRAMAKINI (Ilala).

Wito huo umetolewa na Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa katika Kata ya Pangani iliyopo Ilala jijini Ilala alipokuwa akifunga awamu ya pili ya huduma za mkono kwa mkono maarufu 'Ones Stop Center' zinazotembea kwa waathirika wa unyanyasaji na ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika kata tisa za Mkoa wa Kipolisi wa Ilala takribani kwa siku 18.

Amesema kuwa, vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto na unyanyasaji watoto vikiwemo vya ubakaji, ukeketaji, utumikishaji watoto na ndoa za utoto vinavyowanyima watoto haki zao haviwezi kukubalika, kwani watoto hao ndio viongozi na wajenzi wa taifa la kesho.

“Watoto wa sasa ndio akina Rais Samia Suluhu wa kesho, ndio akina Lazaro Mambosasa wa kesho, ndio madaktari na viongozi wa kesho hivyo, lazima haki zao zilindwe na waendelezwe.Hivyo, lazima Watanzania tuungane na kusimama pamoja kuhakikisha wanawake na watoto wanalindwa ili kesho na kesho kutwa, washike nafasi mbaimbali kutumikia taifa,”amesema.

Aidha, Kamanda Mambosasa ameipongeza Taasisi ya Fredrich Naumann Foundation for Freedom East Africa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kufanikisha huduma za mkono kwa mkono zinazotembea na kuahidi kuendelea kuunga mkono na kusaidia kufanikiwa zaidi kwa huduma hizo ili kukomesha vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia eneo lake.

Mkurugenzi wa Programu wa Fredrich Naumann Foundation for Freedom East Africa kwa Tanzania na Kenya, Veni Swai akizungumza katika hafla hiyo, alilipongeza Jeshi la Polisi kwa jitihada za kupambana na uhaifu ukiwemo ukatili wa kijinsia na hasa utaratibu wa kuwafuata wananchi mahali walipo pamoja na kutoa elimu na huduma dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Alisema, hatua hiyo inaifanya jamii kuongeza imani yake kwa polisi hivyo, kujitokeza kueleza kero zao zikiwemo za kifamilia.

“Kitendo cha polisi kuwafuata wananchi katika maeneo yao na kusikiliza kero zao sambamba na kuwapa msaada ukiwemo wa kisheria, msaada wa kipolisi, unasihi na huduma za afya na elimu dhidi ya ukatili wa kijinsia, kinaonesha uhusiano mwema baina ya polisi na raia unazidi kuimarika. Bado wadau wote kwa pamoja tuna kazi kubwa mbele yetu na sisi tunaahidi kuendelea kushirikiana na polisi kadiri inavyowezekana,"alisema Swai.

Naye Naye Mratibu wa One Stop Center katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Dkt.Christina Onyango amesema, mbali na vituo hivyo kutoa huduma za upimaji afya kama macho, sukari na shinikizo la damu, unasihi, huduma za kisheria, pia wananchi wamekuwa wakifundishwa namna ya kubaini, wahusika, dalili, aina na namna ya kuripoti na kutunza ushahidi dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Dkt.Onyango alimebainisha kuwa, awamu ya kwanza ya huduma kama hizo ilifanyika Desemba, mwaka jana katika kata saba zilizopo katika mkoa huo wa kipolisi ikiwa ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.

Post a Comment

0 Comments