Watu 30 mbaroni kwa tuhuma za kumiliki shamba kubwa la bangi, kuvunja nyumba,wizi wa pikipiki

Watu 30 mkoani Rukwa wamekamatwa na Jeshi la Polisi katika operesheni maalumu iliyofanyika mwezi huu, anaripoti Mwandishi Diramakini (Rukwa).

Watu hao wanatuhumiwa kwa makosa tofauti likiwemo la kumiliki shamba la bangi mkoani hapa.

Kaimu Kamanda wa polisi mkoani haa, Theopister Mallya amesema kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakikabiliwa na makosa ya kuvunja na kuiba, wizi wa pikipiki huku wengine wakikutwa wanamiliki shamba lenye ukubwa wa heka moja na nusu wakiwa wamelima bangi.

Amesema kuwa, operesheni hiyo ilifanyika katika maeneo tofauti ya mkoa huo ambapo Katika tukio la kwanza watu 15 waliokua wakijihusisha na vitendo vya kuvunja nyumba za watu na kuiba walikamatwa wakiwa na Mali za wizi pamoja na vifaa wanavyotumia wakati wakivunja.

Kaimu Kamanda Mallya amesema kuwa katika tukio la pili watu watatu walikamatwa na pikipiki tano za wizi zenye namba za usajili MC 596 CDL aina ya Star, MC 220 AXG aina ya Star, na MC 285 CMX aina ya Kinglion.

Pia amesema kuwa, pikipiki nyingine ni zenye namba za usajili T 218 BSQ aina ya T- Better, pamoja na pikipiki isiyo na namba za usajili yenye Chasis namba MG 2A211B2zewb79630 na Injini namba kl157FM13J26038 aina ya Boxer.
Kamanda Mallya amesema kuwa, katika tukio la mwisho watu 12 walikamatwa wakiwa wanamiliki shamba la bangi hekari 1.5 pamoja na bangi kavu yenye uzito wa kilo 25 wakiwa wamezihifadhi ndani.

Amesema kuwa, watu hao wamekuwa wakiuza madawa hayo ya kulevya katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Rukwa.

Hata hivyo, amesema watuhumiwa wote hao wanashikiliwa na watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa awali utakapokamilika.

Post a Comment

0 Comments