Acheni kupanga safu za uongozi, Chongolo awaonya wana CCM

Na Dismas Lyassa, Kibaha

KATIBU Mkuu wa CCM Taifa, Daniel Chongolo amewaonya wana CCM kuacha kupanga safu za uongozi badala yake walekeze nguvu katika kutekeleza ilani ya chama hicho ili wananchi waweza kutimiziwa ahadi ambazo zilitolewa katika uchaguzi wa mwaka jana.

Akizungumza katika Mkutano wake alioufanya katika viwanja vya CCM Mkoa wa Pwani, Kibaha Mjini leo, Chongolo amesema "Ni kweli unaweza kuwa unampango wa kugombea Ubunge au nafasi yoyote, sio kosa, bali kila kitu kina wakati wake. Huu ni wakati wa utekelezaji wa kutekeleza kile ambacho CCM kiliahidi kwa wananchi.

"Wakati ukifika unaweza kuchukua fomu, lakini tusitumie nguvu kuharibiana na kuja na ajenga ambazo hazina mashiko kwa maendeleo ya wananchi na ustawi wa chama. Watanzania wanataka utekelezaji wa Ilani, hilo ndilo la msingi kwa sasa," akasema Chongolo.

Katibu mkuu huyo alikwenda mbali zaidi na kuwaasa wana CCM kuelekeza nguvu zao katika kuangalia ahadi zote zilizotolewa na CCM na kuhakikisha zinatekelezeka kadri inavyowezekana, ili kufanya wananchi kuendelea kukiamini chama cha Mapinduzi.

"Lakini pia nataka kuona katika mikutano yetu, katika vikao vyetu kama chama tunakuja na hoja zinazojibu kero za wananchi, kama ni eneo halina maji, barabara nk tunahitaji kuona chama kinashirikiana na Serikali katika kutambulia kero za wananchi na kushauri au kufuatilia utatuzi wa kero hizo," anasema Chongolo na kuongeza kuwa hapendi kuona chama kinajadali mambo ya watu binafsi na masuala binafsi, badala yake kijikite zaidi kujadili kero za wananchi na namna ya kuzipatia majibu kwa kushirikiana na Serikali.

Kauli hiyo ilisababisha kulipuka kwa furaha kutoka kwa washiriki wa mkutano huo ulioshirikisha viongozi wakuu wa chama na Serikali mkoa, wilaya, kata na mitaaa mbalimbali katika mkoa wa Pwani, huku baadhi yao wakisikika wakisema kuwa anachokisema ni ukweli kwamba baadhi ya viongozi wanaonekana kupanga safu katika uchaguzi wa CCM ambao unatarajiwa kufanyika mwakani katika ngazi tofauti katika chama hicho.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news