ATCL yasitisha safari za India

Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) limetangaza kusitisha safari zake kwenda nchini India ambako vifo na maambukizo ya virusi vya corona (Covid-19) yanazidi kuongezeka, ANARIPOTI MWANDISHI DIRAMAKINI.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na afisa mtendaji mkuu wa shirika hilo, Ladislaus Matindi inasema safari hizo zimesitishwa kuanzia leo Mei 4,2021.

“ATCL itaondoa faini zote kutokana namabadiliko haya, itatoa tiketi nyingine au kuwarudishia nauli zao abiria waliokuwa wamekata tiketi,” amesema Matindi.

Aidha,ili kupata ufafanuzi zaidi, Matindi amewataka abiria waliokata tiketi kupiga namba O800110045 bure.Hayo yanajiri ikiwa Shirika la Afya Duniani ((WHO) limesema kuwa, janga la virusi vya corona (COVID-19) limeendelea kuwa jinamizi kwa India likiongeza idadi ya wagonjwa wapya kila siku kati ya 350,000 na 400,000 huku wengine kwa maelfu wakipoteza maisha.

Takwimu za shirika hilo zinaonyesha kwamba karibu watu 220,000 wameshapoteza maisha hadi sasa kwa COVID-19 India huku wagonjwa waliothibitishwa wakikaribia milioni 20.

Katika mahojiano na Mwandishi wa Habari wa Umoja wa Mataifa India, Anshu Sharma, Mkuu wa WHO nchini humo, Dkt. Roderico H. Ofrin amesema “Nadhani ni muhimu kutambua kwamba mwezi kama wa Februari hivi maisha yalirejea katika hali ya kawaida, shughuli za kiuchumi na kijamii zikaanza kuendendelea kama kawaida, lakini pia tumeshuhudia watu kutozingatia masharti ya kukabiliana na COVID-19 na hayo yamevipa virusi fursa na fasi za kuendelea kusambaa. Ingawa kuna sababu nyingi lakini kubwa ni kwamba tumevipa virusi fursa ya kuendelea kuambukiza”

Dkt. Ofrin alisema ni muhimu hatua zote zikaendelea kuzingatiwa ikiwemo kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka, umbali kati ya mtu na mtu, upimaji na zaidi ya hayo,“Kuna nyenzo nyingine ya kukabili janga hili ambayo ni chanjo. Hivyo India imeweza kutoa chanjo kwa watu milioni 165 hadi sasa . 

Hii ni njia nyingine ambayo kwa hakika itasaidia kukomesha maambukizi ya mlipuko huu wa pili kama wanavyouita wa COVID-19.”

WHO na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kushirikiana kwa karibu na mamlaka nchini India ili kuhakikisha maambukizi mapya yanakomeshwa na maisha ya watu yanaokolewa.

Post a Comment

0 Comments