CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA KAHAMA (KACU) CHAWALIPA MALIPO YA PILI WAKULIMA WA PAMBA

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Kahama

Chama Kikuu Cha Ushirika Kahama (KACU) kimewalipa malipo ya pili wakulima wa Pamba waliouza Pamba msimu wa mwaka 2019/2020.
Mgeni rasmi-Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe Anamringi Macha (Kulia) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe Nyabaganga Taraba (Kushoto) mfano wa hundi wa malipo ya pili ya Pamba kwa wakulima wa Wilaya ya Kishapu wakati wa hafla ya makabidhiano hayo yaliyofanyika tarehe 18 Mei 2021 Mjini Kahama Mkoani Shinyanga. (Picha Zote Na Mathias Canal).

Akizungumza leo tarehe 18 Mei 2021 katika hafla ya kukabidhi fedha hizo kwa wakulima wa Pamba iliyofanyika katika Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga, Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Tanzania Marco Mtunga amekipongeza Chama Kikuu Cha Ushirika Kahama (KACU) kwani kimekuwa chama mkombozi katika zao la Pamba nchini.

Kadhalika Mtunga amesema kuwa kiasi cha Fedha kitatengwa kwa ajili ya Tume ya Maendeleo ya ushirika ili Afisa Ushirika aweze kuzungukia Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) mara kwa mara kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali kwenye AMCOS badala ya kusubiri mwisho wa msimu.

Amesema kuwa Bodi ya pamba Tanzania imekusudia Kutumia mahakama inayotembea ili kuwabaini wabadhilifu wa mali za Ushirika na kuwachukulia hatua za haraka.
Mgeni rasmi-Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe Anamringi Macha akisisitiza jambo wakati wa hafla ya kukabidhi malipo ya pili ya Pamba iliyofanyika tarehe 18 Mei 2021 Mjini Kahama Mkoani Shinyanga.
Mwenyekiti wa KACU Ndg Emmanuel Cherehani akisoma taarifa ya chama hicho mbele ya mgeni rasmi wakati wa hafla ya kukabidhi malipo ya pili ya Pamba iliyofanyika tarehe 18 Mei 2021 Mjini Kahama Mkoani Shinyanga.
Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Tanzania Ndg Marco Mtunga akisisitiza jambo mbele ya mgeni rasmi wakati wa hafla ya kukabidhi malipo ya pili ya Pamba iliyofanyika tarehe 18 Mei 2021 Mjini Kahama Mkoani Shinyanga.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe Nyabaganga Taraba akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi malipo ya pili ya Pamba iliyofanyika tarehe 18 Mei 2021 Mjini Kahama Mkoani Shinyanga.
Akisoma taarifa ya chama hicho Mwenyekiti wa KACU Ndg Emmanuel Cherehani amesema kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020 Mfuko wa Pembejeo ulikosa Fedha za kuhudumia zao hilo hivyo KACU walifanikisha kukopa Tsh Bilioni 8 iliyopelekea kupatikana kwa pembejeo ambazo zilitumika katika msimu wa mwaka 2020/2021.

Amesema kuwa Chama hicho kimetekeleza vyema majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuwalipa wakulima malipo ya awali na hatimaye kimefanikiwa kuwalipa malipo ya pili jambo ambalo huenda likapelekea katika miaka ijayo wakulima wakaweza kulipwa malipo ya awamu ya tatu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe Nyabaganga Taraba amewasisitiza wakulima wa Pamba nchini kusimamia ubora wakati wote wa msimu wa kilimo kwani kufanya hivyo kutaongeza wigo wa kuingiza pato kubwa wakati wa uuzaji wa Pamba.

Amesema kuwa vipo vyama vingi vya Kilimo lakini vimeshindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo hivyo amevitaka kutumia nafasi zao kujifunza kupitia KACU.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news