China yapongezwa kwa kuendeleza utamaduni wa kuinga mkono Zanzibar

Na Diramakini (diramakini@gmail.com)

Rais ya Jamhuri ya Watu wa China imepongezwa kwa kuendeleza utamaduni wake wa kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo mikakati iliyowekwa katika kuimarisha uchumi wa Buluu.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa pongezi hizo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China Zhang Zhisheng, aliyefika Ikulu kwa ajili ya Kujitambulisha.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Balozi Mdogo wa Jamhuri ya Watu wa China anayefanyika Kazi zake Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng, alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha Mei 19,2021, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Jamhuri ya Watu wa China ni mdau muhimu wa maendeleo ya Zanzibar kwani imekuwa ikiiunga mkono Zanzibar tokea miaka ya 60 mara baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.

Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi huyo mdogo wa China anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Zhang Zhisheng kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamani sana juhudi za Serikali ya China katika kuunga mkono miradi mbali mbali ya maendeleo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Jamhuri ya Watu wa China imeweza kuunga mkono sekta mbali mbali za maendeleo hapa Zanzibar ikiwemo afya, elimu, kilimo, viwanda na nyenginezo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar ina furahishwa na juhudi za nchi hiyo za kuendeleza uhusiano na ushirikiano wake katika kuendeleza na kuimarisha sekta za maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Jamhuri ya Watu wa China katika kuhakikisha sekta za maendeleo zinaimarika sambamba na kuimarisha udugu na urafiki uliopo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi huyo mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika suala zima la ujenzi wa Bandari mpya ya Mangwapwani na kuwakaribisha wawekezaji pamoja na Kampuni kutoka China kuja kuekeza Zanzibar.

Mapema Balozi mdogo wa China Zhang Zhisheng alimueleza Dk. Mwinyi kuwa Jamhuri ya Watu wa China inathamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na kuahidi kuendeleza kwa manufaa ya pande zote mbili.
Balozi Zhisheng alimueleza Rais Dk. Mwinyi kuwa Jamhuri ya Watu wa China iko tayari kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukuza uchumi wake kupitia dira ya uchumi wa buluu pamoja na kulipokea wazo la kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini humo.

Katika maelezo hayo, Balozi huyo alieleza kwamba China ni miongoni mwa nchi za mwanzo kuyatambua Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, na kuanzia hapo ikiwa nchi ya kwanza kuleta wataalamu wakiwemo madaktari wa fani mbali mbali pamoja na wataalamu wa sekta za maendeleo na viwanda wakiwemo wataalamu wa kilimo.

Balozi Zhisheng alitumia fursa hiyo kumpongeza kwa mara nyengine tena Rais Dk. Mwinyi kwa niaba wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Xi Jinping kwa kuchaguliwa na wananchi wa Zanzibar kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kishindo.

Aidha, Balozi Zhisheng alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kusimamia vyema Serikali ya Umoja wa Kitaifa anayoiongoza na kueleza matumaini yake ya kwamba Zanzibar itapiga hatua kubwa ya maendeleo kutokana na mshirikiano makubwa yaliopo.

Pamoja na hayo, Balozi huyo amemuahidi Rais Dk. Mwinyi kwamba watalii kutoka Jamhuri ya Watu wa China wataongezeka kwa wingi kuja kuitembelea Zanzibar kwani kinachozuia hivi sasa ni kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa COVID 19 duniani.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Afrika Dk. Nyamajeje Calleb akiwa amefuatana na uongozi wa Benki hiyo ambapo alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake hasa kupitia uchumi wa buluu.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuipongeza Benki hiyo kwa kuonesha utayari wake wa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi katika kuimarisha uchumi wake hasa katika sekta ya uchumi wa buluu ambayo inajumuisha utalii, uvuvi pamoja na mafuta na gesi asilia.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi aliueleza uongozi huo hatua zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza katika kukuza uchumi wake ikiwa ni pamoja na mikakati iliyowekwa na Serikali anayoiongoza katika ujenzi wa bandari kubwa ya kisasa ya Magwapwani sambamba na hatua zilizowekwa katika kukukuza uchumi wa buluu.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Afrika Dk. Nyamajeje Calleb alimueleza Rais Dk. Mwinyi historia ya kuanzishwa kwa Benki hiyo hapa nchini pamoja na shughuli zake inazozifanya ikiwa ni pamoja na kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Alimueleza Rais Dk. Miwnyi jinsi Benki hiyo inavyofanya shughuli zake katika kuwasaidia wananchi katika miradi yao ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo pamoja na kushirikiana na Serikali katika kuimarisha baadhi ya miradi ya maendeleo

Post a Comment

0 Comments