CRDB yawaita wawekezaji

BENKI ya CRDB imesema kuwa inao mtaji wa kutosha wa kuwazesha wafanyabiashara, wakulima,wafugaji,wavuvi watakaokuja kuwekeza katika Mkoa wa Mara hivyo wajitokeze kuchangamkia fursa hiyo, anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini) Mara.Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta.

Imesema kuwa iko tayari muda wote kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwainua wananchi wafikie uchumi bora kwa kuwapa mikopo itakayowawezesha kufanya shughuli za uzalishaji.

Kauli hiyo imetolewa Mei 28, 2021 na Meneja wa CRDB Kanda ya Ziwa, Lusingi Sitta Wakati akitoa mada kwenye kongamano la uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji Mkoa wa Mara lililofanyika ukumbi wa Mwembeni Complex Mjini Musoma, na kuwakutanisha wadau mbalimbali kutoka Serikalini na taasisi binafsi.

Meneja huyo amesema kuwa, CRDB imejizatiti kikamilifu kuona inachangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Mara hasa kwa kutoa mikopo kwa makundi yote ili kuyawezesha kutumia fursa za kiuchumi zilizoko mkoani humo.

"Benki ya CRDB inao mtaji mkubwa ambao unaweza kuwakopesha wafanyabiashara na makundi mengine yatakayokuja kufanya shughuli za uwekezaji katika Mkoa wa Mara. Tutahakikisha tunaunga mkono kwa dhati jitihada za Serikali katika kuinua maisha ya wananchi na pato la Mkoa na Tanzania kwa ujumla,"amesema.

Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mara, Boniface Ndengo amesema benki ya CRDB ni mdau muhimu kwa Maendeleo ya Mkoa wa Mara. Hivyo akawahimiza wafanyabiashara, wawekezaji, kutoka ndani na nje ya mkoa kuitumia ili kuweza kupata mitaji ya kuendesha shughuli zao.

Aidha, Ndengo ameongeza kuwa, TCCIA ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuwapa elimu na miongozo ya kibiashara ili waweze kuzifanya kwa ufanisi ili kulinda mitaji yao na kuweza kurejesha mikopo hiyo bila kuyumba kibiashara.

Akizindua Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Mara, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alisema Mkoa wa Mara ni sehemu salama ya kufanya uwekezaji kwa kuwa inazo fursa mbalimbali ikiwemo ziwa Victoria, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, maeneo mengi ya migodi, ardhi yenye rutuba kwa ajili ya shughuli za kilimo chenye tija.

Pia, Waziri Mkuu Majaliwa alizishukuru Taasisi za Kifedha ikiwemo benki ya CRDB kwa kuwa tayari kuweza kuwawezesha Wawekezaji watakaokuja kuwekeza Mkoani Mara. Huku akiwataka viongozi wa Serikali ndani ya mkoa huo kusimamia mwongozo huo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news