DC ATAKA WAZAZI WALIOZUIA WATOTO KUMEZA DAWA TIBA KINGA YA MINYOO NA KICHOCHO WATOE MAELEZO

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt.Vincent Anney Naano amezindua zoezi la ugawaji wa dawa za minyoo na kichocho aina ya Albendazole na Praziquantel kwa ajili ya tiba kinga kwa Wanafunzi wa Shule za Msingi zilizopo katika Manispaa ya Musoma, anaripoti Amos Lufungulo (Diramakini) Mara.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Anney Naano akimpa dawa mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwisenge wakati wa zoezi la uzinduzi wa zoezi hilo kwa Manispaa ya Musoma.Pembeni mwake ni Mganga Mkuu wa Manispaa ya Musoma, Dkt.Sisti Mosha. (Picha zote na Diramakini).

Akizindua zoezi hilo leo Mei 25, 2021, katika Shule ya Msingi Mwisenge 'A' mkuu huyo wa wilaya amesema, watoto wote ambao hawatapata fursa ya kumeza dawa hizo wazazi wao wanapaswa kufika shuleni kutoa maelezo kwani umezaji wa dawa hizo ni lazima na siyo hiari kwa mujibu wa maagizo ya Serikali.

Amesema, tabia ya baadhi ya Wazazi na Walezi kuzuia watoto wao kumeza dawa hizo ni kosa kwani Serikali imetumia fedha nyingi kuwezesha zoezi hilo ili kuwakinga Watoto na magonjwa ya kichocho na minyoo.

"Nitoe agizo kwa Walimu wote mhakikishe Watoto wanakunywa dawa hizi tumieni daftati la mahudhurio kuhakikisha Watoto wote wamemeza dawa. Dawa hazina madhara, lakini cha ajabu Wazazi wengine wamezuia watoto kuja shuleni kumeza dawa hizi,"amesema Dkt.Naano.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Wizara ya Afya anayesimamia zoezi hilo kwa Mkoa wa Mara amesema, dawa hizo zimegharimu fedha nyingi kwa lengo la kuwakinga Watoto hao. Amesisitiza Wazazi kutokuwa na hofu kuhusiana na dawa hizo kwani ni salama kwa matumizi.

"Watoto wengi wanapougua kichocho na minyoo huwa hawaoneshi dalili badala yake madhara ndio hujitokeza,Serikali imeamua kugawa dawa hizi ili kuwakinga. Niwaombe wazazi wasiwe na hofu kwani zipo hata hospitalini zimekuwa zikitolewa," amesema Dkt. Ludamila.

Naye Mganga Mkuu wa Manispaa ya Musoma, Dkt.Sisti Mosha amesema kuwa zoezi hilo la ugawaji wa dawa hizo litafanyika kwa shule za Msingi 55 za Manispaa ya Musoma ambapo walengwa ni Wanafunzi 42,893 wenye umri kati ya miaka 5-14 ambapo Wazazi wao wamechangia chakula ili Wanafunzi wapate kula ndani ya saa mbili kabla ya kunywa dawa.

Ameongeza Kuwa, Manispaa ya Musoma ni miongono mwa Halmashauri 9 za Mkoa wa Mara zinazotekeleza Mpango wa kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ambayo yamo hasa katika Jamii maskini ambapo Jamii hata Wataalamu husika au Viongozi hawayapi umuhimu kulingana na madhara yake katika Jamii.

Ameyataja Magonjwa hayo kuwa ni pamoja na matende,mabusha,trakoma,kichocho, usubi, na minyoo ya tumbo. Huku akibainisha kuwa katika Manispaa ya Musoma zoezi hilo litahusisha kukinga na kutibu Magonjwa mawili ambayo ni kichocho na minyoo ya tumbo ambayo yamethibitika kuwepo katika Mkoa wa Mara.

Ameongeza kuwa, dawa ambazo wanapewa Wanafunzi zimethibitishwa na Wizara ya Afya kuwa ni salama na hazina madhara na pia zimethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mamlaka ya Dawa Tanzania (TMDA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news