DUWASA YAJA NA MIRADI MIKUBWA YA MAJITAKA


MAMLAKA ya Majisafi Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imesema ipo kwenye hatua za awali za utekelezaji wa miradi mikubwa ya upanuzi wa mtandao wa majitaka ili kuendana na kasi ya ukuaji wa jiji hilo baada ya Serikali kuhamia rasmi.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini humo kuhusu maendeleo na mipango ya Mamlaka hiyo katika kutoa huduma za majisafi na majitaka jijini humo.

Alitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa mabwawa mapya 16 katika eneo la Nzuguni B ambapo imeshalipa fidia ya eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 60 ambapo kiasi cha Sh. milioni 600 zimelipwa fidia.

Joseph alisema mabwawa yaliyopo Swaswa kilometa zipatazo sita (6) toka mjini. Mabwawa haya yapo manne (4) kila moja likiwa na ukubwa wa meta 200 X 200.

"Tuna Mradi wa Kujenga Mabwawa ya Kutibu maji 16, na kwa sasa tuna Mabwawa Manne ambayo yamezidiwa uwezo hivyo tunaenda kujenga mabwawa hayo 16 kwenye eneo la Nzuguni B na tayari tumeshalipa fidia ya eneo hilo lenye ukubwa wa Hekari 60 ambalo limegharimu Zaidi ya Milioni 600 kulipata," alisema Mhandisi Joseph.

"Gharama za utekelezaji wa mradi huo ni kiasi cha Bilioni 161 sawa na Dola za Marekani Milioni 70 ambazo ni mkopo wa gharama nafuu kutoka serikali ya Korea, na Mradi huu upo katika hatua nzuri na tumeshirikiana na wizara ya maji na wizara ya fedha kuhakikisha mahitaji yote muhimu yanapatikana," alisema.

Alisema mitandao ya kukusanyia majitaka imeenea kikamilifu (comprehensive reticulation sewers network) kwenye maeneo matatu tu ya mji.

Maeneo hayo ni Mlimwa West (Area C), Mlimwa East (Area D) na Central Business Area. Maeneo mengine ya mji yaliyofikiwa na mtandao wa kukusanyia majitaka japo kwa kiasi kidogo ni kata za Makole, Viwandani, Madukani, Kizota, Chamwino, Kikuyu Kaskazini, Uhuru na Tambukareli.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news