HOPE FOR GIRLS AND WOMEN TANZANIA WAENDELEA KUWAPIGA MSASA WAKULIMA, WAGAWA SIMU JANJA MKOANI MARA

Katika kuhakikisha wakulima wanalima na kuzalisha kwa tija,Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania limeendesha mafunzo ya siku mbili ya kilimo cha kisasa kwa wakulima 20 wa Kijiji cha Kinyariri Kata ya Buhemba Wilaya ya Butiama pamoja na kuwagawia simu janja 20 bure zenye thamani ya shilingi milioni 10 ambazo zitawasaidia kutambua magonjwa mbalimbali yanayokabili mazao yao, ANARIPOTI AMOS LUFUNGULO (DIRAMAKINI ) Kanda ya Ziwa.
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania Rhobi Samwelly (katikati) akiwaelekeza Wakulima namna ya kutumia Simu Janja kutazama katika mmea iwapo umeathiriwa na Wadudu. (PICHA NA AMOS LUFUNGULO (DIRAMAKINI ).

Mafunzo hayo yamefanyika Mei 3 hadi 4, 2021 na kuhusisha wataalamu wa kilimo kutoka Wilaya ya Butiama ambapo yana lengo la kuwawezesha kuendesha shughuli zao za kilimo kwa ufanisi pamoja na kutoa elimu hiyo kwa wakulima wengine katika maeneo yao ili kuongeza uzalishaji wa mazao kwa ubora unaotakiwa.

Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly ambaye amewahi kutunukiwa Tuzo ya Heshima ya Malkia wa Nguvu kutokana na juhudi zake za kutetea haki za binadamu na kupambana na ukatili wa kijinsia, amesema wameamua kutoa elimu hayo na simu hizo zilizounganishwa na teknolojia ya kisasa ili kuwapa wakulima maarifa yatakayowasaidia kutambua magonjwa ya mazao mbalimbali na namna ya kukabiliana nayo kabla hayajaleta athari.

Wakulima wa Kijiji cha Kinyariri wakiwa katika shamba wakifanya mazoezi ya vitendo kwa kutumia simu janja kutambua iwapo viwavijeshi vimeathiri mimea hiyo.Kulia ni Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly.(PICHA NA AMOS LUFUNGULO (DIRAMAKINI ).
 
Pia, Rhobi amewaasa wakulima hao, kuunga mkono mapambano ya ukatili wa kijinsia kwa kuhimiza usawa hasa katika umiliki wa rasilimali baina ya mwanamke na mwanaume ngazi ya familia ikiwemo kufanya maamuzi ya pamoja katika matumizi ya mazao yanayozalishwa kwa manufaa ya wote.

"Mkulima akienda na simu yake shambani akaiweka kwenye mmea atatambua ugonjwa huo na kuchukua hatua ya kuwaona wataalamu. Na pia kila mkulima aliyepata elimu hii na simu atakwenda kuunda kikundi cha wakulima wenzake kuanzia 10 ili kuwapa elimu. Mkulima akiwa na mazao mazuri hata ukatili wa kijinsia unapungua katika familia shabaha yetu kubwa ni kuona ukatili unaisha kutokana na uzalishaji wenye tija katika ngazi ya familia,"amesema Rhobi.
Afisa Kilimo wa Wilaya ya Butiama, Revocatus Rutunda akitumia simu janja kubaini viwavijeshi vamizi katika mahindi wakati wa semina ya wakulima wa Kijiji cha Kinyariri iliyoendeshwa na Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania.(PICHA NA AMOS LUFUNGULO (DIRAMAKINI ).
 
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Wilaya ya Butiama Revocatus Rutunda amelipongeza Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania kwa kutoa simu hizo kwa wakulima hao.

Ambapo amesema zitasaidia kuongeza uzalishaji kwa tija kwa wakulima hao na hivyo kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia ndani ya wilaya hiyo.

Rutunda ameongeza kuwa, katika mafunzo hayo wakulima wamefundiashwa magonjwa mbalimbali yanayokabili zao la Muhogo ikiwemo batobato kali, michirizi kahawia, utitiri pamoja viwavijeshi vamizi upande wa mahindi sambamba na kufanya mazoezi ya kutumia Simu hizo ili kuwawezesha kupata ujuzi thabiti utakaowawezesha kuzitumia wakiwa katika maeneo yao kugundua iwapo mazao yao yanakabiliwa na wadudu.

"Jumla ya simu 40 tumepokea kwa awamu mbili katika Wilaya ya Butiama, ambapo Kata ya Kukirango simu 20 na Kata ya Buhemba simu 20. Tumekubaliana na wakulima waliopata simu hizi wanakwenda kuunda vikundi na kila kikundi kitakuwa na watu 10. Kwa maana hiyo tutakuwa na jumla ya wakulima 400 na elimu hii itaendelea kutolewa lengo ni kuona wakulima wanazalisha mazao yao kwa tija ili kuinua uchumi,"amesema Rutunda.

Aidha Rutunda, amewaomba wakulima hao kwenda kuzitumia simu hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.amewahimiza wawe mabalozi katika kuwaelimisha wengine kwa ufanisi ili kuhakikisha kilimo kinakuwa na mchango katika kukuza katika uchumi wao.

Kwa upande wake Isack Nyanza mkulima wa Kijiji cha Kinyariri, amesema atahakikisha anaelimisha Wakulima wengine kupitia mafunzo aliyoyapata. Na kupitia simu hiyo, amesema itawanufaisha wakulima wengi kukabiliana na Magonjwa mbalimbali katika eneo lake.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kinyariri, Winfrida Wangwe amesema wananchi hawakuwa na uelewa mzuri kutambua magonjwa mbalimbali yanayokabili mazao kutokana na uchache wa wataalamu. Lakini kupitia mafunzo hayo wameelimika na pia amewaomba wakulima hao kuwa sehemu ya kushiriki kuongeza uzalishaji wa kisasa.

Post a Comment

0 Comments