Katibu Mkuu wa BAWACHA Catherine Ruge amwangukia Rais Samia teuzi

Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA (BAWACHA), Catherine Ruge amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan kuongeza idadi ya kuteua wanawake katika nafasi mbalimbali za kiuongozi nchini, anaripoti AMOS LUFUNGILO (Diramakini) Mara.

Amesema, licha ya Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuingia madarakani kuahidi kuwateua wanawake katika nyadhifa mbalimbali za uongozi kwa kuzingatia vigezo, bado idadi ya wanawake aliowateua haiendani na wanaume waliopo katika nafasi mbalimbali za uongozi kwa sasa.

Baada ya kikao hicho, Kaimu Mwenyekiti BAVICHA, Sharifa Suleiman na Katibu Mkuu, Catherine Ruge waliingia mtaani kusajili wanachama kwenye Mfumo wa #TunasongaKidigitali mjini Musoma.

Ruge ameyasema hayo mjini Musoma Mkoa wa Mara wakati akizungumza katika mkutano wa chama uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ngazi ya wilaya, Kanda ya Serengeti , mkoa na makao makuu chini ya Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa lengo la kukijenga chama hicho na kukiimarisha.

Katibu Ruge amesema kuwa, wanawake wana mchango mkubwa katika maendeleo mbalimbali kuanzia ngazi ya familia, kata, tarafa, wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla.

Hivyo amemuomba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aongeze idadi ya wanawake katika kuwateua ili waweze kuwatumikia Watanzania.

‘’Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aongeze idadi ya kuteua viongozi wanawake katika kulitumikia Taifa, kwa mfano ameteua makatibu tawala 28, lakini wanawake ni 11 tu na hata wakurugenzi wa halmashauri nchini ni 191 lakini wanawake ni 36 pekee. Mawaziri ni 23, lakini wanawake mawaziri ni 5 pekee, makatibu wakuu wa wizara ni 29, wanawake ni watano,"amesema Katibu Ruge.

Katibu huyo wa BAWACHA Taifa ameongeza kuwa, katika nafasi yake ya Ukatibu wa BAWACHA Taifa, atahakikisha anapigania haki za wanawake, usawa, haki, demokrasia pamoja na kuwaunganisha wanawake ndani ya chama hicho wawe na sauti moja katika kulinda usawa kama ambavyo mikataba mbalimbali ya kimataifa inaelekeza na ambayo Tanzania ilisaini.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa BAWACHA Taifa, Nuru Ndosa amewataka wanawake ndani ya chama hicho kuunga mkono kwa dhati mchakato wa kudai katiba mpya na tume huru ya uchaguzi huku akiongeza kuwa atafanya ziara magereza mbalimbali hapa nchini ili kujionea wanawake waliofungwa iwapo walikuwa na makosa ambayo yaliwatia hatiani.

Post a Comment

0 Comments