KMC FC KUSHUKA DIMBA LA CHAMANZI JUMAMOSI KUWAKABILI AZAM FC

Mara baada ya kutoka sare dhidi ya Namungo, Kikosi cha KMC FC kimendelea kujifua kuelekea katika mchezo wake mwingine wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara dhidi ya Azam utakaopigwa siku ya Jumamosi Mei 15 katika uwanja wa Chamanzi.
Mchezo huo ambao KMC FC itakuwa ugenini, utachezwa saa 16:00 jioni ambapo hadi sasa kikosi hicho kinaendelea kufanya maandalizi yake ya mwisho ili kuhakikisha kwamba inakwenda kufanya vizuri katika mchezo huo muhimu.

Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni Chini ya Kocha Mkuu John Simkoko na msaidizi wake Habibu Kondo wameendelea kukiandaa kikosi hicho ili kuhakikisha kwamba ushindi unapatikana licha ya kuwepo na ushindani kwa timu zote mbili mkubwa na hivyo kuondoka na alama tatu muhimu.

”Tumetoka kwenye mchezo ambao tulikuwa ugenini dhidi ya Namungo, na sasa tunajiweka tayari kwenye mchezo mwingine, tunakutana na Azam FC ambayo kimsingi ni bora, inauwezo mkubwa, lakini hata ukiangalia kikosi chetu kiko bora zaidi, na kikubwa tunakwenda kupambania alama tatu ambazo hata wao wanazihitaji.

Ukiangalia hata kwenye msimamo wa Ligi, wapo nafasi ya tatu na sisi tupo kwenye nafasi ya tano, lakini pia katika mchezo uliopita tulipata ushindi wa goli moja tukiwa kwenye uwanja wetu wa nyumbani, hivyo licha ya kwamba tunaenda ugenini bado tunajiamini kwakuwa tunauwezo mkubwa wa kupambana na yoyote kwa ajili ya maendeleo ya Timu yetu.

Imetolewa leo Mei 12

Na Christina Mwagala

Afisa Habari na Mahusiano wa KMC FC

Post a Comment

0 Comments