Kocha wa Real Madrid Zinedine Zidane ajiuzulu

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Zinedine Zidane ambaye ni kocha wa Real Madrid amejiuzulu kwa mara nyingine kukifundisha kikosi hicho.

Uamuzi huo ameufikia siku chache baada ya Real Madrid kushindwa kuchukua ubingwa wa Ligi ya La Liga na kuruhusu watani wao wa jiji Atletico Madrid kuondoka na kombe hilo.

Ushindi ambao ulimfanya mshambuliaji wa Atletico Madrid, Luis Suarez kumwaga machozi wakati timu yake hiyo ikitwaa ubingwa wa La Liga.

Matokeo hayo waliyapata katika dimba la Jose Zorrila baada ya Valladolid kupata bao moja huku Ateltico Madrid wakipata 2.

Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulikuwa ni wa maamuzi ambapo Oscar Pilano alianza kuwafunga Atletico dakika ya 18 na Angelle Correa dakika ya 57 alisawazisha na dakika ya 67 Suarez alifunga bao la ushindi na kumfanya afunge jumla ya mabao 21 ndani ya La La Liga kwa msimu wa 2020/21.

Suarez nyota wa zamani wa Barcelona alishangazwa na kitendo cha mabosi wa timu hiyo kumfungulia mlango na kumtaka aondoke katika timu hiyo msimu uliopita na aliamua kwenda Atletico Madrid bure kwa kuwa mkataba wake ulikuwa umekwisha jambo ambalo lilikuwa linamuumiza kwa kuwa alishushwa thamani yake ndani ya Barcelona.

Baada ya mchezo wao wa mwisho na kuthibitishwa kwamba Atletico Madrid ni mabinhwa wa La Liga, Suarez alikuwa mpole na kusema kuwa Barcelona hawakumthamini kwa kuwa walimuondoa licha ya kuwa alikuwa akijituma.

Atletico Madrid imetwaa ubingwa huo ikiwa na jumla ya alama 86 ikifuatiwa na Real Madrid ambao wapo nafasi ya pili na alama 84 huku Barcelona ya Lionel Messi ikiwa nafasi ya tatu na alama 79 wakati timu iliyocheza na Suarez ikiwa nafasi ya 19 na alama 31.

Kutokana na matokeo hayo, ndiyo,Real Madrid imethibitisha uamuzi huo wa Zidane na kusema kwenye taarifa yake kuwa, “sasa ni wakati wa kuheshimu uamuzi wake na kuonyesha kuthamini taaluma yake, kujitoa na mapenzi yake kwenye klabu katika kipindi chote.”

Mfaransa huyo alikuwa na mkataba hadi Juni 2022, lakini alikuwa tayari ameripotiwa kwamba alikuwa akiwaambia wachezaji wa Real Madrid kwamba mapema Mei, mwaka huu ataondoka klabuni hapo, wakati msimu wa 2020-21 utakapomalizika.

Aidha, kwa nyakati tofauti kama kocha wa Real Madrid, Zidane alishinda Ligi ya Mabingwa
mara tatu na ligi ya Uhispania mara mbili, lakini ilimaliza msimu huu bila ya kombe lolote, ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 11.

Hata hivyo, taarifa hiyo imesema Zidane ni miongoni mwa wachezaji watakaoendelea kuthaminiwa sana wakati wote na kuongeza kuwa anajua kwamba ni miongoni mwa wachezaji walioko kwenye mioyo ya mashabiki wa klabu hiyo na Real Madrid itabakia kuwa nyumbani kwake wakati wowote hata atakapoondoka.
Zinedine Zidane. (Picha na Football Espana).

Post a Comment

0 Comments