Mbunge Mtenga ampongeza Makamu wa Rais kwa maagizo ya neema kwa wakulima

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MBUNGE wa Jimbo la Mtwara Mjini, Hassan Mtenga amempongeza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Mpango kwa kuziagiza kampuni zote zinazoagiza mbegu mbalimbali kutoka nje ya nchi kuzalisha hapa nchini ili kuwezesha uwekezaji wa ndani.

Maagizo hayo ya Mei 27, mwaka huu yalienda sambamba na maelekezo kwa wakuu wa taasisi za Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutakiwa kujizatiti na kujipima katika kuzalisha mbegu bora zitakazoweza kutosheleza na kumfikia mkulima.

Dkt.Mpango ameyasema hayo kwenye Siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Kumbukizi ya Kifo cha Hayati, Edward Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Kwanza wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mjini Morogoro.
Mbunge Mtenga amesema, maagizo ya Makamu wa Rais yanatoa faraja kubwa kwa wakulima ambapo asilimia kubwa ya Watanzania wamejikita katika shughuli za kilimo kwa ajili ya uzalishaji wa chakula, kipato na kujiajiri.

Katika maagizo hayo, Makamu wa Rais Dkt.Mpango alisema, “Napenda nichukue nafasi hii kuzitaka kampuni zote ambazo zinaagiza mbegu kutoka nje kuzalisha mbegu hapa nchini na Wizara ya Kilimo ijipange kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo haya na wasisubiri tuwaulize,"alisema.

Huku, Mbunge Mtenga akisema kuwa,maagizo hayo baada ya kuyasikia yalimpa faraja kubwa akiamini kuwa, sasa wakulima nchini watanufaika kwa wingi kutokana na ukweli kwamba uzalishaji wa mbegu hizo hapa nchini utazingatia mazingira na ubora wa hali ya juu hivyo kuwawezesha wakulima kunufaika zaidi.

"Awali ya yote nichukue nafasi hii kumpongeza sana Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Philip Isdor Mpango kwa maagizo hayo muhimu ambayo ni neema kwa wakulima na yanalenga kukipaisha kilimo chetu hapa nchini.

"Hii inadhirisha wazi namna ambavyo Serikali yetu ambayo inaongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilivyodhamiria kumkomboa mkulima ili aweze kuzalisha kwa faida zaidi. Pia nichukue nafasi hii kuwapa changamoto wataalam wa kilimo kuingia mashambani, kutafiti aina gani ya mazao ya kimkakati ambayo yanastawi kulingana na kanda zetu.

"Hii itafungua fursa nyingi za kilimo na uzalishaji wenye tija zaidi, mfano kule kwetu Mtwara, wengi wamezoea kusikia korosho, kumbe mihogo, ufuta, mpunga na mazao mengine yanastawi sana, hivyo wakitafiti kwa kina watabaini aina ya mazao ili uzalishaji wa mbegu bora ukifanyika uweze kuelekezwa kulingana na maeneo kwa ajili ya kuleta matokeo makubwa,"amesema Mtenga.

Post a Comment

0 Comments