Mkurugenzi Jiji la Dodoma atatua mgogoro wa ardhi uliodumu miaka 30

Na Dennis Gondwe, DODOMA

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru ametatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 30 katika Mtaa wa Ndachi na kuwawezesha wananchi kupata hati za kumiliki maeneo yao kwa mujibu wa sheria.

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru akiongea kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Mtaa wa Ndachi, Kata ya Mnadani jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mafuru ametatua mgogoro huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa michezo katika Mtaa wa Ndachi uliopo Kata ya Mnadani jijini hapa.

Mafuru amesema kuwa, wananchi hao wamekosa maendeleo kwa muda mrefu kutokana na kuwa na migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu.

Mafuru amesema kuwa, wananchi wakitaka migogoro hiyo ya ardhi iishe, inaisha na pia wasipotaka migogoro iishe pia haiwezi kuisha. “Hivyo, ni vema kuchukua uamuzi wa kumaliza migogoro hiyo kwa wakati unaotakiwa ili kuweza kuleta maendeleo zaidi katika mtaa huo.

“Sehemu nyingine tumeweza kumaliza migogoro kwa kutoa majina ya watu 100 alafu wanakuja ofisini tunatatua matatizo yao, pia wakimaliza wanafata wengine 100 tena wanafuata 100 mpaka wanaisha na migogoro pia inaisha. Hapa pia tutafanya hivyohivyo. Ili kumaliza tatizo ni vyema kulifuata tatizo na sio kulikimbia. Maeneo mengi tumeweza kumaliza migogoro hii ikiwemo Nzuguni, Mtumba, Michese pamoja na Nala. Wananchi wamepata haki zao, lakini Ndachi wamechelewa kutokana na migogoro iliyopo inatakiwa kuisha kwanza,” amesema Mkurugenzi Mafuru.

Amesema kuwa, wakati wa upimaji walikubaliana watagawana asilimia 30 kwa Jiji na asilimia 70 kwa wananchi. Asilimia 30 ya Jiji itatumika kuwafidia wananchi ambao viwanja vyao vitakuwa vimeingia katika miundombinu kama barabara, shule na vituo vya afya.

Amesema kuwa, orodha ya majina ya wananchi pamoja na ramani za viwanja hivyo zimekamilika. 

“Tutahamishia ofisi hapa. Wataalam wetu watakuwepo hapa ili kutatua kero zote za wananchi hatua kwa hatua mpaka pale watakapozimaliza. Sisi tumekuja kulinda ardhi ya wananchi kutoka kwenye ardhi ya maneno maneno na kuwa mali halali ambayo inaitwa hati. Hii ni ardhi salama kwa manufaa ya wananchi na vizazi vyao vijavyo,"amesema Mkurugenzi Mafuru.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango miji na Mazingira ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Jafari Mwanyemba alisema kuwa wanaelekea ukingoni mwa zoezi hilo. “Ramani pamoja na majina tayari Tumeshatoa. Kazi imeandaliwa na wataalamu ambao ni binadamu hivyo, kama kuna kasoro ni vizuri zikatajwa ili kutatuliwa mapema. Kama una eneo haki haitapotea, tutahakikisha kila mtu anapata haki yake na migogoro kuisha kabisa. Niwasihi tu kufuata vile ambavyo mtakuwa mkiambiwa wakati wa kukamilisha zoezi hilo’’ alisema Mwanyemba.

Nae mkazi wa mtaa huo, Sharifa David alipongeza juhudi za halmashauri katika kutatua mgogoro huo uliodumu muda mrefu. Alisema kuwa wanaweza kuendeleza maeneo yao na kujiletea maendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news