NAIBU WAZIRI WAITARA ATAKA TATHMINI MV MBEYA II

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mwita Waitara, amezitaka taasisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Wakala wa Meli (TASAC), Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kufanya tathmini ya kina kabla ya kuanza matengenezo ya meli ya MV Mbeya II.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akimsikiliza Kapteni Kalendelelo Pastory (kulia) wa Meli ya MV Mbeya II, alipokagua meli hiyo bandarini Kiwira, Wilayani Kyela, Mkoani Mbeya.

Ametoa kauli hiyo wilayani Kyela baada ya kukagua miundombinu katika bandari za Kiwira na Itungi na kubaini ucheleweshaji wa matengenezo ya Meli hiyo iliyosimama kutoa huduma katika Ziwa Nyasa mapema mwezi Aprili kutokana na hitilafu za kifundi.

“Meli hii imesimama zaidi ya wiki tatu sasa na ninajua meli hii bado iko kwenye muda wa uangalizi hivyo ninawaagiza TPA, TASAC, DMI na Kampuni ya Songoro kukaa na kuwasilisha ripoti haraka iwezekaavyo ili matengenezo yaanze” ameagiza Naibu Waziri Waitara.

Naibu Waziri Waitara amesema fedha za Serikali zilizowekezwa kwenye ujenzi wa meli zilirahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kwa wananchi wanaozunguka Ziwa Nyasa kwa nchi za jirani na kuitaka TPA kurejesha huduma mapema iwezekanavyo.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akitoa Maelekezo kwa Uongozi wa Kampuni ya Songoro Marine iliyojenga Meli ya MV Mbeya II, wakati alipokagua chelezo katika bandari ya kiwira, Wilayani Kyela, Mkoani Mbeya.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Waitara imeitaka Kampuni ya Songoro Marine kufanya tathmini ya Chelezo ambayo imekuwa bandarini Kiwira kwa zaidi ya mwaka bila kufanyiwa matengenezo ili kujiridhisha na ufanisi wake kabla ya kupandisha meli zinazohitaji matengenezo.

Akiwasilisha taarifa yake kwa Naibu Waziri Waitara Kaimu Meneja wa Bandari katika Ziwa Nyasa Abdallah Mohammed amesema kuwa tangu kuanza kutumika kwa meli ya MV. MBEYA II kumekuwa na changamoto mbalimbali za kiufundi ambazo Mamlaka imekuwa ikielekeza Kampuni ya Songoro kuzirekebisha.
Muonekano wa Meli ya MV Mbeya II ikiwa imepaki kusubiri matengenezo katika bandari ya Kiwira mara baada ya kupata hitilafu za kiufundi na kusitisha huduma mapema mwezi Aprili, Wilayani Kyela, Mkoani Mbeya.

“Mamlaka ya Bandari ilileta wataalamu kukagua Meli hii na walibaini kuwepo kwa hitilafu kwenye baadhi ya mifumo na imekuwa ikirekebishwa mara kwa mara”. Amesema Mohamed.

Meli ya MV Mbeya II ni moja ya meli tatu ambazo zimejengwa na TPA kwa fedha za ndani lengo likiwa ni kuboresha usafirishaji wa abiria na mizigo Ziwa Nyasa, meli nyingine ni pamoja na MV. RUVUMA na MV. NJOMBE.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news