Nyayo inayoaminika kuwa ya Yesu kivutio adimu cha utalii Litembo

KIJIJI cha Litembo kilichopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma kimebarikiwa kuwa na vivutio adimu cha utalii ambavyo huwezi kuviona mahali pengine popote, anaripoti Albano Midelo (Ruvuma).
Nyayo iliyokanyagwa juu ya mwamba wa jiwe Litembo wilayani Mbinga ni kivutio kikubwa cha utalii.

Salvius Nyamajabeni ni Mwenyekiti Baraza la Mila na Utamaduni wa kabila la wamatengo katika kijiji hicho aliyechaguliwa tangu mwaka 1958 anasema,Kijiji hicho kina kivutio ambacho kinawashangaza wengi ambacho anakitaja kuwa ni uwepo wa nyayo ya binadamu wa kale ambayo wananchi wa Litembo wanaamini kuwa ni nyayo ya Yesu.

“Kuna alama ya nyayo ya binadamu yenye vidole ambayo imekanyagwa juu ya jiwe miaka mingi iliyopita,sisi wananchi wa Litembo tunaamini kuwa Yesu amekanyaga kwa sababu haifutiki miaka yote’’,anasema Nyamajabeni.
Vivutio vya aina mbalimbali vilivyopo katika jiwe la Litembo,ukiwemo mnara wa makumbusho ambao umejengwa kuwakumbuka watu 800 waliouawa na wajerumani mwaka 1902.

Anasema kila mwaka waumini wa kikristo wanapanda juu kilele cha jiwe la Litembo ambako kuna nyayo na kwenda kuhiji na kwamba eneo hilo pia limewekwa msalaba.

Mwenyekiti huyo anasema kijiji cha Litembo kina vivutio vingi vya utalii ambavyo havijatangazwa na kufahamika ambapo amelitaja jiwe la Litembo,lina utajiri wa utalii wa kishujaa na kihistoria kutokana na mababu na mabibi zetu takribani 800 waliuwawa na wakoloni wa kijerumani Machi 4,1902,kutokana na kukataa kutawaliwa.
Nyayo na bindamu ambao wakazi wa Litembo Mbinga wanaiita kuwa ni nyayo ya Yesu ,ni miongoni mwa kivutio cha utalii wa kihistoria.

Amelitaja jiwe ambalo yalifanyika mauaji hayo linaitwa Litembo,jina ambalo limetokana na kufanana sana na kichwa cha mnyama tembo.

Anasema eneo hilo yalikuwa makazi na maficho ya wazee wakati wa vita dhidi ya wajerumani ambapo ndani ya jiwe hilo kuna pango refu linalotokea katika Kijiji cha Maguu wilayani Mbinga.Inaelezwa ndani ya pango hilo kuna Wanyama wakali,nyoka,maji mengi,pia inadaiwa kuna madini ya zebaki na samani za chuma.

Katibu wa Baraza la Mila na Utamaduni Kata ya Litembo, Bruno Tembo anasema mashujaa hao 800 baada ya kuuawa walizikwa katika makaburi ya Pamoja ya watu 25 katika Kijiji cha Litembo na kwamba ili kuwakumbuka mashujaa hao mnara wa makumbusho umejengwa kwenye maeneo ya jiwe la Litembo na kwamba kila mwaka Novemba 28 yanafanyika maadhimisho ya kuwakumbuka wazee 800 waliopambana na wajerumani.
Mwenyekiti Mstaafu wa kijiji cha Litembo Paulo Mwingira anasema serikali ya kijiji hicho kwa kushirikiana na wazee wa mila wa kabila la wamatengo wamejipanga kuhakikisha kuwa vivutio vyote vya utalii wa kihistoria na kishujaa vilivyopo katika eneo hilo vinalindwa na kuendelezwa kwa ajili ya urithi wa kizazi cha sasa na kijacho.
Afisa Maliasili na Utalii Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema,wamedhamiria kuvitangaza vivutio vya utalii wa kihistoria na kishujaa vilivyopo eneo la Litembo ili watalii wengi waweze kufika na kuona namna mababu zetu walivyoshiriki katika harakati za ukombozi dhidi ya wakoloni wa kijerumani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news