RAIS DKT.MWINYI AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA MCHEZAJI WA KIMATAIFA WA TIMU YA CRYSTAL PALACE

Na MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza azma ya Mchezaji wa timu ya mpira wa miguu wa Klabu ya Crystal Palace inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza (EPL) Mamadou Sakho ya kuanzisha kituo cha kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana hapa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi hizo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mchezaji wa timu ya mpira wa miguu wa Kilabu ya Crystal Palace inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza (EPL) ambaye pia ni Mchezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa Mamadou Sakho.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mchezaji wa Kimataifa wa Timu ya Crystal Palace ya Uingereza Mamadou Sakho akiwa na Mkewe. Majda Sakho,alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yalionyika katika ukumbi wa Ikulu leo 1-6-2021.   

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba azma hiyo ni mwanzo mzuri katika kuinua na kuendeleza vipaji vya michezo vya vijana wa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alimpongeza Mamadou kwa kuitembelea Zanzibar kwa mara ya pili kutokana na mazingira pamoja na watu wa Zanzibar na utamaduni wao.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimueleza mchezaji huyo wa timu ya Crystal Palace kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana nae katika kuanzisha kituo hicho cha kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana hapa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Mchezaji wa Kimataifa wa Timu ya Crystal Palace ya Uingereza. Mamadou Sakho akiwa na mkewe Majda Sakho, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alimueleza mchezaji huyo kuwa ujio wake una umuhimu mkubwa katika kuutangaza utalii wa Zanzibar pamoja na vivuto vilivyopo.

Nae Mchezaji wa timu ya mpira wa miguu wa Kilabu ya Crystal Palace inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza (EPL) ambaye pia ni Mchezaji wa timu ya taifa ya Ufaransa Mamadou Sakho alimueleza Rais Dk. Mwinyi azma yake ya kuanzisha kituo cha kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana hapa Zanzibar.

Mamadou ambaye amefuatana na Mkewe Majda Sakho, alisema kuwa ameamua kuchukua hatua hiyo ya kuanzisha kituo cha kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana hapa Zanzibar kwa kutambua kwamba ana deni na wajibu mkubwa wa kuleta maendeleo Afrika akijuwa kwamba yeye ni Mwafrika licha ya kwua amezaliwa Ufaransa na anabeba uraia wa Taifa hilo.

Aliongeza kuwa ameichagua Zanzibar kuwa ni eneo maalum kwa kuanzisha kituo hicho kitakachoendeleza soka hapa nchini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi ya mlango wa Zanzibar mgeni wake Mchezaji wa Kimataifa wa Timu ya Crystal Palace ya Uingereza Mamadou Sakho akiwa na mkewe Majda Sakho, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na kuagana mgeni wake mchezaji wa Kimataifa wa Timu ya Crystal Palace ya Uingereza, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)

Alisema kuwa vipaji vitakavyotolewa katika kituo hicho itakuwa ni alama maalum aliyoiacha katika kuinua soka na kuithamini asili yake. “Ninapokuwa Ulaya sio wengi wanaoniuliza unatoka nchi gani ya Ulaya bali huniuliza ninatoka nchi gani ya Afrika, najivunia asili yangu ya Afrika, hivyo nimeamua kuifanyia kitu na nimeichagua Zanzibar”,alisisitiza Mamadou

Sambamba na hayo, Mamadou alieleza jinsi alivyovutiwa na mazingira na anavyoipenda Zanzibar kutokana na ukarimu wa watu wake, mazingira pamoja na utamaduni wake.

Mchezaji huyo pia, alieleza azma yake ya kujifunza lugha ya Kiswahili na kueleza kuwa tayari ameshaanza kujifunza na kumueleza Rais kwamba mara ijayo atakapokuja basi atazungumza kwa lugha ya Kiswahili.

Baada ya kuzungumza na Rais Dk. Mwinyi, mchezaji huyo pia alipata fursa ya kufanya mahojiano na waandishi wa Habari waliohudhuria katika mazungumzo hayo ambapo katika maelezo yake amelezea utayari wake wa kuwa Balozi wa Hiyari wa Kuutangaza Utalii wa Zanzibar.

Nae Waziri Utalii na Mambo ya Kale Leila Muhamed Mussa alisema kuwa mchezaji huyo nguli wa soko duniani amekuja Zanzibar kiutalii kwa ajili ya kuitangaza Zanzibar lakini pia ana azma ya kuifanyia kitu Zanzibar ambacho ni kuanzisha kituo cha kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana wa Zanzibar.

Alieleza kuwa kwa vile maisha yake yote ameitumia katika mchezo wa mpira wa miguu hivyo alisema lazima zawadi ambayo amekuwa nayo kwenye maisha ni kuitunuku Zanzibar kwa kujenga kituo hicho ambacho kitakuwa cha kisasa na maalum kwa vijana kuwakuza kimichezo.

Waziri huyo kwa upande wake alieleza utayari wa Serikali kupitia Wizara yake pamoja na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo mbali ya kujenga majengo pia, aliahidi kuleta wataalamu wa kutoa mafunzo ya mpira wa miguu kwa vijana.

“Hivyo tunaposema neena tupu sasa tutambue kwamba hizo ndio neema zenyewe tunazozisema”. Alisisitiza Waziri Leila.

Mamadou ambaye ni raia wa Ufaransa amewasili Zanzibar mnamo Mei 29, 2021 kwa ziara ya siku nne akiwa ameambatana na familia yake ambapo tangu alipowasili ameshatembelea Ukanda wa Utalii wa Mashariki, kituo cha kulelea watoto yatima cha SOS kilichopo Mombasa, Unguja, Mji Mkongwe wa Zanzibar pamoja na kijiji cha Nungwi.

Aidha, Timu ya Waandishi wa habari wa Televishen ya TF1 ya nchini Ufaransa imefuatana na mchezaji huyo maarufu kwa lengo la kutengeneza makala maalumu ya ziara yake itakayotumika kuutangaza utalii wa Zanzibar kwenye soko la utalii la Ufaransa hususan maeneo ya vivutio vya utalii aliyotembelea.

Wanamichezo, wasanii pamoja watu mbali mbali maarufu duniani wamekuwa wakiitembelea Zanzibar mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kutembelea vivutio vya utalii, ziara hizo za watu mashuhuri ni fursa adhimu ya kuitangaza Zanzibar kiutalii hasa kwa wale wenye wafuasi wengi katika mitandao yao ya kijamii ambayo ni nyenzo muhimu yenye kufikifiksha ujumbe kwa watu wengi ndani ya muda mfupi.

Familia ya beki wa kimataifa wa Ufaransa, Mamadou Sakho iliwahi kutembelea Zanzibar mnamo Juni mwaka 2017 wakati huo mchezaji huyo akichezea timu ya Liverpool ya England na kutembelea kituo cha kulelea watoto yatima cha SOS kilichopo Mombasa, Unguja.

Post a Comment

0 Comments