RC Makalla atoa maagizo nane kwa viongozi Dar

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amefanya kikao na wakuu wa wilaya, wakurugenzi na makatibu tawala na kuwapatia maagizo nane ya kushughulikia ikiwemo suala la usafi wa jiji la Dar es salaam.

RC Makalla akizungumza na wakuu wa wilaya, wakurugenzi na makatibu tawala Mei 28, 2021 mkoani Dar es Salaam.

RC Makalla amesema, ajenda ya usafi ni moja ya vipaumbele muhimu alivyopanga kuanza navyo ambapo ametaka kila halmashauri kuhakikisha kampuni zinazopewa tenda ya usafi ziwe na sifa ikiwemo kuwa na vitendea kazi vya kutosha.

Aidha, RC Makalla amewaagiza kuja na mpango mkakati wa kubaini maeneo gani Wamachinga watapangiwa wafanye biashara zao bila kuvunja sheria na kushangazwa na tabia ya wanaofanya biashara kwenye maeneo hatarishi ikiwemo juu au chini ya miundombinu ya maji, umeme na gesi.

Pamoja na hayo, RC Makalla amewaelekeza viongozi kuanzia ngazi ya Wilaya, Kata na Mitaa kushughulikia mtandao wa ombaomba jijini humo kwa kubaini mawakala wanaowaleta na maeneo wanapowahifadhi ili kutokomeza kabisa suala hilo.

Hata hivyo, RC Makalla ameelekeza wakuu wa wilaya kuhakikisha wanashughulikia kero za migogoro ya ardhi na kubainisha kuwa ataanza ziara ya kila kata.

Kuhusu suala la elimu, Mkuu wa Mkoa ametaka kila halmashauri kuweka makadirio ya wanafunzi wanaoandikishwa na watakaofaulu ili kuanza mapema maandalizi ya ujenzi wa madarasa na madawati jambo litakaloepusha uhaba wa vyumba vya madarasa na madawati.

RC Makalla pia ametoa maelekezo kwa viongozi wote kuhakikisha wanatokomeza suala la uhalifu katika maeneo yao na kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mapema pindi wanapowabaini wahalifu katika maeneo yao.

Sanjari na hayo ametaka kila Halmashauri kuhakikisha zinazingatia takwa la kisheria kwa kutenga asilimia 10 ya mikopo kwa vijana, walemavu na wazee.

Mbali na hayo RC Makalla amesema Vita ya dawa za kulevya Jijini humo ni ajenda endelevu huku akiwahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwaibua Wauzaji ili kuwanusuru vijana wanaoangamia kila siku kwa matumizi ya dawa hizo.

Post a Comment

0 Comments