SHILATU AKEMEA UPIGAJI MIRADI YA UJENZI

Na Mwandishi Wetu, Mihambwe

Afisa Tarafa Mihambwe wilayani Newala Mkoa wa Mtwara, Emmanuel Shilatu amekemea vikali tabia ya hujuma ya upigaji na uchezeaji wa miradi ya ujenzi ya kimaendeleo.
Hayo yamejitokeza kwenye ziara aliyoifanya Gavana Shilatu ya kutembelea mradi wa ujenzi Zahanati ya Miuta ambao haujanza kutumika lakini "gypsum boards" zimeanza kuanguka zenyewe huku nyaya za umeme zikitandazwa pasipo kuwekwa kwenye bomba.

"Mwenyekiti ujenzi huu una mashaka, unaona mwenyewe jengo halijaanza kutumika tayari "gypsum boards" zimeshaanza kuanguka, nyaya hazijapita kwenye bomba na nyie mpo mkishuhudia haya ambapo kimsingi ni mradi wenu. Hili halikubaliki, lazima haya madudu yarekebishwe,"amesema Gavana Shilatu.

Gavana Shilatu aliamua kuwatuliza Wananchi waliokuwa na hasira kwa kusisitiza upigaji hautavumilika ndani ya Tarafa ya Mihambwe na atazidi kuanika madudu endapo wanaopewa dhamana hawatajirekebisha na kusisitiza ujenzi urudiwe.

"Haiwezekani Watu walioharibu kule ndio hao hao wanaharibu na huku, sitovumilia madudu haya ambayo hata Wananchi hawayapendi, ni shetani pekee anaweza kuvumilia ubadhirifu huu. Hivyo marekebisho ya haraka yafanyike na Wananchi mtulie kila kitu Serikali itasimamia ipasavyo na tuendelee kushirikiana,"amesisitiza Gavana Shilatu.

Mwenyekiti Kijiji cha Miuta Ndugu Hamad Asali aliwaeleza Wananchi kuwa hawakubaliani na madudu hayo na watasimamia ujenzi huo urudiwe ipasavyo ndio wakubali kuupokea.

"Mradi huu unaendelea kujengwa na pale penye mapungufu tunaendelea kuwakaba Mafundi warekebishe ndipo tuupokee," amesisitiza Mwenyekiti wa Kijiji Miuta Ndugu Asali.

Akizungumza kwa niaba ya Wananchi Ndugu Muhibu Ally Lisakasi alifurahishwa na ujio wa Afisa Tarafa Mihambwe ambapo amepata fursa kueleza kero za mradi huo na kutamani uishe kwa haraka na ufanisi ili uanze kutumika.

"Nimefurahi sana kutembelea walau na kiongozi wa ngazi ya juu kwani hili la Zahanati ni kero kwetu, tunataka ujenzi mzuri ukamilike na jengo lianze kutumika. Afisa umetufurahisha sana kututembelea leo kwani tunapata fursa kueleza shida zetu na utatuzi tunaupata, Mwenyezi Mungu azidi kukubariki,"amesema Ndugu Lisakasi.

Katika ziara hiyo Gavana Shilatu aliambatana na Mwenyekiti Kijiji, Mtendaji Kijiji, kamati ya ujenzi, fundi pamoja na Wananchi waliojitokeza kueleza kero zao mara baada ya kumuona Afisa Tarafa Mihambwe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news