Simba SC yawagomea Kaizer Chiefs, yawapindua...Msuva atokea benchi hadi Nusu Fainali

Na Diramakini (diramakini@gmail.com)

Wekundu wa Msimbazi Simba SC wameendeleza rekodi yao ya nyumbani kwa leo Mei 22, 2021 kutimiza zaidi ya siku 2,970 ikiwa ni zaidi ya miaka nane bila kupoteza ikiwa nyumbani, Dar es Salaam.
Hayo yamedhihirika leo baada ya kuimiminia mabao matatu kwa tasa timu ya Kaizer Chief kutoka nchini Afrika Kusini.

Ni katika mchezo uliochezwa katika dimba la Benjamin William Mkapa lililopo Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam ikiwa ni marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ushindi wa leo kwa Simba SC licha ya kuwa mnono, haukuwawezesha kusonga mbele kutokana na mtanange wa awali huko nchini Afrika Kusini Kaizer Chiefs iliwatandika mabao 4 kwa tasa.

Kwa matokeo hayo, Simba SC imeondolewa katika michuano hayo ikiwa imeonyesha kabumbu safi.

Waliochana nyavu za Kaizer Chief leo ni pamoja na Nahodha John Bocco alidondosha mawili na Clatous Chama alifunga mahesabu kwa kuweka nyavuni bao la tatu.

Kutokana na matokeo hayo, kwa sasa Kaizer Chief wanaungana na watetezi Al Ahly ya Misri iliyolazimisha sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambayo ilikubali kichapo cha 2-0 kwenye mechi yao ya kwanza

Wakati huo huo, mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva ametokea benchi zikiwa zimesalia dakika tatu na kuiwezesha klabu yake, Wydad Athletic kutinga Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya MC Alger Uwanja wa Mohamed V mjiniCasablanca, Morocco.

Msuva ambaye ni mchezaji wa zamani wa Yanga SC ya nyumbani Tanzania, aliingia dakika ya 87 kuchukua nafasi ya Aymane Hassouni kabla ya Walid El Karti kuifungia bao pekee Wydad dakika ya 90 kwa matokeo hayo wanakwenda Nusu Fainali kwa ushindi wa jumla wa 2-1 kufuatia sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Algiers.

Muda si mrefu tutakujulisha kati ya Esperance ya Tunisia itakapoialika CR Belouizdad kutoka nchini Algeria kati yao ni yupi ambaye ataingia nusu fainali.

Post a Comment

0 Comments