Timu ya Lipuli FC yapewa fedha maandalizi Mechi ya Jumamosi

Na CATHERINE MBIGILI, Iringa

MKUU wa Mkoa Wa Iringa,Queen Sendiga ametoa kiasi cha fedha shilingi milioni moja na nusu kwa wachezaji wa timu ya Lipuli FC ili zikawasaidie katika mechi yao ya siku ya Jumamosi wanapokwenda kuikabili timu ya Fountaine gate ya mkoani Dodoma.

Fedha hizo amezitoa alipokutana na timu hiyo baada ya kuahidi kukutana nayo wakati alipokuwa katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM ) mkoani hapa.

Ameeleza kuwa, anajua timu ina shida hasa kwenye masuala ya kifedha hivyo akisema atoe hela ikawasaidia atakuwa anadanganya lakini anawapatia pesa kidogo ili wakishinda mechi atarudi ili waongee makubwa zaidi.

"Nawapatia wachezaji milioni moja na nusu najua kiasi hiki cha fedha hakiwezi kikatosha, lakini najua itawasaidia kwenye bajeti yenu ya usafiri itakayo pungua najua mtaongeza nyinyi wenyewe,"amesema Queen.

Pia Mkuu huyo aliahidi kuwa,baada ya mechi ya Jumamosi atakutana na timu hiyo tena ili waweke mipango mikakati itakayoisaidia timu hiyo kurudi kwenye nafasi yake kama hapo awali.

"Naomba tukacheze kwa moyo wa dhati kabisa kwa faida ya wana Iringa ninaiona taswira mbele zuri sana ya michezo mimi binafsi napenda michezo na ninapenda kuona mafanikio ya mpira kwa sababu nina amini kuna vitu vingi sana kwenye mpira ambavyo vinaonekana na vingine havionekani, lakini vyote vinapatikana kwenye soka,"amesema Mkuu wa Mkoa.

Amesema, binafsi anatamani kuiona timu hiyo ikicheza na timu kubwa kama Simba,Yanga au Azam mkoani hapo kama zilivyo timu za mikoa mingine.

"Ninaamini hizi sura ninazoziona hapa kwanza wote bado wadogo damu zinachemka lazima mfanye vizuri,"amesema.

Naye Mwalimu wa timu hiyo Meja Mstaafu Mingange, yeye alisema anashukuru kwa fedha hizo zilizotolewa anaimani ujio wa mkuu huyo wa mkoa utaongeza hamasa katika mechi iiyoko mbele yao na wao wataenda kupambana ili waweze kuibakisha timu katika ligi na kujiandaa kwa msimu ujao.

Amesema, kama timu ina wachezaji wa kutosha wapo vizuri wanaujua mpira vizuri na imani take ni kwamba watapata matokeo mazuri.

Amesema, wana changamoto ya timu kukosa wafadhili hivyo kupelekea timu kukosa pesa ya kujiendesha,pamoja na posho na mchezaji akikosa pesa hata uwanjani hawezi kufanya vizuri.

"Tumeweza kujitahidi licha ya mazingira ya timu kuwa magumu kama unavyoona hali halisi tunapambana kwa ajili ya kuiweka timu iweze kukaa sehemu zuri,"amesema.

Post a Comment

0 Comments