UTEUZI WA HOYCE TEMU KUWA BALOZI NA UELEWA WETU KUHUSU MABALOZI

Na Abbas Mwalimu (0719258484)

Jumapili tarehe 23 Mei, 2021 

Jumamosi tarehe 22 Mei, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alifanya uteuzi wa mabalozi 23, miongoni mwa mabalozi wateule hao wamo Hoyce Temu aliyewahi kuwa Miss Tanzania mwaka 1999, Togolani Mavura ambaye ni msaidizi wa Rais wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Macocha Tembele aliyewahi kuwa Msaidizi wa Hayati Benjamin William Mkapa na Kaimu Idara ya Ushirikiano wa Kikanda, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Luteni Jenerali Yakub Hassan Mohammed ambaye ni Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ.

Hoyce Temu.

Kati ya wateule hao 23 wa Rais Samia Suluhu Hassan wateule wawili wameonekana kugusa akili za watu wengi sana katika mitandao ya kijamii, hawa ni Hoyce Temu na Luteni Jenerali Yakub Mohammed.

Kwa lengo la kufahamu kuhusu uteuzi wa Hoyce Temu na Lt. Jen Yakub Mohammed katika jicho la kidiplomasia ni vema tukafahamu tafsiri ya Balozi.

Balozi ni "mwakilishi anaetumwa na Mkuu wa nchi, Serikali ama taasisi ya kimataifa kwenda kumuwakilisha Rais, mkuu wa serikali au taasisi au nchi inayomtuma katika nchi inayompokea." 

Mabalozi hufanya kazi zao kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 unaohusu Mahusiano ya Kidiplomasia (Vienna Convention on Diplomatic Relations of 1961) ambapo kazi za ubalozi zimeelezwa katika Ibara ya 3.

Wanapokuwa katika nchi walizotumwa mabalozi huwa na kazi za kukusanya taarifa mbalimbali na kuzituma nyumbani sambamba na kulinda maslahi ya Tanzania na watanzania katika nchi wanazowakilisha.

Lakini si mabalozi wote huteuliwa na kutumwa katika nchi mbalimbali duniani, wapo ambao huteuliwa na Mheshimiwa Rais na kuendelea kufanya shughuli zao hapa nchini.

Ili kufahamu hili ni vema kwanza tuangalie uteuzi wa mabalozi, huwaje?

Mabalozi kama walivyo wateule wengine huteuliwa kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 sambamba na marebisho yake yote. Ibara ya 36 (2) ya Katiba inasomeka kama ifuatavyo:

"Rais atakuwa na madaraka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali, na watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi hizo katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, nafasi ambazo zimetajwa katika Katiba hii au katika sheria mbalimbalizilizotungwa na Bunge kwamba zitajazwa kwa uteuziunaofanywa na Rais."

Katika muktadha wa uteuzi wa mabalozi unatokana na katiba na Rais huweza kumteua yeyote kuwa balozi itakavyompendeza kwa kuzingatia vigezo mahsudi. Kwa kawaida  huwa  kuna mabalozi wa aina mbili:

(1) Wanaoteuliwa kutokana na utashi wa kisiasa (Political Appointees/Diplomats)

(2) Wanaoteuliwa kutokana na weledi wao (Career Diplomats). 

Katika teuzi za aina zote hizo mbili hufanyika kwa siri kubwa mno ambapo kama mteule anatokana na weledi wake kwenye diplomasia yaani kutokana na kuwa Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje (FSO), jina lake hupelekwa kwa siri na Wizara Ikulu na pia kama hatokani na kuwa Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje jina hupelekwa kwa siri na idara ya Usalama wa Taifa kwa ajili ya kuchunguzwa ama kufanyiwa vetting.

Hawa wanaoteuliwa kutokana na utashi wa kisiasa huwa ni pendekezo la Mheshimiwa Rais moja kwa moja kutokana na atakavyoona inafaa kwa kuzingatia wakati, mahitaji, taaluma katika eneo fulani, malengo na mazingira yanayozunguka hali ya halisi ya dunia kwa wakati huo. 

Kwa mfano Rais huweza kuteua Balozi mwenye taaluma katika eneo la Ulinzi na Usalama hapa mara nyingi utakuta Rais akiwateua maafisa wa wa juu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania  (JWTZ) au Jeshi la Polisi kuhudumu nchi ambazo zina changamoto za kiusalama kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Burundi n.k, lakini pia maafisa hao wa jeshi huweza kutumwa katika nchi zilizo kimkakati kama Urusi, Misri, Afrika Kusini na Rwanda.

Si rahisi kwa mtu ambaye si mwanajeshi kuhudumu katika nchi zenye migogoro au vita au zilizo kimkakati zaidi  ambapo kunahitaji utaalamu wa masuala ya vita, migogoro na stratejia ili aweze kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa urahisi. Ndiyo maana tunaona Balozi wetu kule Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ama DRC ni Afisa wa Juu wa Jeshi Luteni Jenerali Meela. Katika muktadha wa aina hiyo hiyo ndipo tunapoona maafisa wa juu kama Luteni Jenerali  Yakub Mohammed Mnadhimu Mkuu wa JWTZ akiteuliwa kuwa Balozi.

Tumeona Rais akizingatia utaalamu katika ulinzi na usalama hata katika uteuzi wa wakuu wa mikoa na wilaya. Kwa mfano, Rais alimteua Kamishna wa Polisi Thobias Andengenye kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,  Brig. Jen. Marco Gaguti kuwa Mkuu wa Mkoa, Balozi Brig. Jen Wilbert Ibuge kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Maj. Jen Charles Mbuge kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera. Ukitazama mikoa hii yote ipo mpakani na ina changamoto za kiusalama kwa mfano Ruvuma na Mtwara kumepakana na nchi ya Msumbiji ambako kuna changamoto ya Ugaidi. Hivyo ni wazi Mheshimiwa Rais anaona ni muhimu kupeleka watu ambao ni  wataalamu kwenye ulinzi katika usalama maeneo hayo.

Kwa upande Hoyce Temu, nadhani wengi hawafahamu kuwa Hoyce Temu alisoma Stashahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Mahusiano ya Kigeni yaani Post Graduate Diploma in Management of Foreign Relations (PGD-MFR) kutoka Chuo cha Diplomasia Kurasini Dar es Salaam ama Mozambique-Tanzania Centre for Foreign Relations (CFR).

Lakini pia wengi huenda  hawafahamu kuwa Hoyce Temu aliwahi kuhudumu Umoja wa Mataifa Tanzania (UN-Tanzania) kama Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano lakini pia alipata kuhudumu kama Mtaalamu wa Mawasiliano UN-Tanzania (UN Communication Specialist) na pia Mchambuzi wa Mawasiliano au UN Communication Specialist.

Hivyo Hoyce Temu ana taaluma ya Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia kutoka Chuo cha Diplomasia na zaidi ya hilo ana weledi wa masauala ya kidiplomasia kutokana na kufanya kazi UN ofisi ya Tanzania.

Alichosoma Hoyce Temu ndicho walichosoma maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ambao kikanuni ni lazima wasome kozi za Chuo cha Diplomasia (CFR) kama kigezo kimojawapo cha kutoka ngazi moja ya daraja kwenda lingine ili waweze kumudu majukumu yao ipasavyo.

Hayo na mengine mengi huzingatiwa pia katika uteuzi wa wale wanaotokana na weledi (Career Diplomats) kama vile kujaza nafasi za ukurugenzi katika idara zilizopo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, baadhi vituo (balozi zilizopo nje) kuwa wazi, wapo mabalozi  waliomaliza muda wakijiandaa kurudi, kuna  kubadilishwa vituo vya kazi na majukumu mengine nchini kwa kadiri Rais atakavyoona inafaa.

Hawa wanaotokana na weledi ni wale ambao wametokea wizara ya mambo ya nje ambao huwa wanapatikana kutokana na kukua katika kazi ama career growth.

Kwa mfano katika Wizara  ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (MFAEAC) ya Tanzania afisa wa Wizara wa Wizara ya Mambo ya Nje (FSO) huwa na mtiririko ufuatao wa ajira kuanzia tangu afisa anaajiriwa mpaka anafikia hatua ya kuteuliwa kuwa Balozi.

Mtu anapoajiriwa katika Wizara ya Mambo ya Nje huanza na cheo cha Third Secretary (TS) cheo hiki katika mfumo wa utumishi (Scheme of Service) hujulikana kama Afisa Mambo ya Nje daraja la Tatu.

Baadae hupanda na kuwa Second Secretary (SS) yaani Afisa Mambo ya Nje Daraja la Pili.

Baadae hupanda na kuwa First Secretary (FS) yaani Afisa Mambo ya Nje Daraja la Kwanza.

Baadae hupanda kuwa Council (Kansela) yaani Afisa Mambo ya Nje Mwandamizi daraja la Pili.

Baadae hupanda kuwa  Minister Council (MC) yaani Afisa Mambo ya Nje Mwandamizi Daraja la Kwanza.

Na mwisho hupanda kuwa Minister Plenipotentiary (MPP) au  Afisa Mambo ya Nje Mkuu (Principal).

MPP ni ngazi ya mwisho ya utumishi katika vyeo vilivyopo Wizara ya Mambo ya Nje ambapo baada ya hapo inatarajiwa mtumishi husika kuweza kuteuliwa kuwa Balozi. 

Lakini pia Rais huweza kumteua hata Afisa Mambo ya Nje Mwandamizi Daraja la Kwanza kuwa Balozi kwa kadiri atakavyoona inafaa kutokana na sababu mbalimbali.

Mabalozi wanaotoka na weledi (Career Diplomats) uteuzi wao hutokana zaidi na mapendekezo ya Wizara ya Mambo ya Nje. 

Tukitazama wengi wa walioteuliwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mabalozi kati ya hawa 23  wametokea ama Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ama Ikulu jambo linaloonesha wazi Mheshimiwa Rais anasimamia kauli yake ya kuzingatia weledi  katika teuzi mbalimbali.

Katika mabalozi hawa walioteuliwa wapo watakaokuwa mabalozi wenye uwezo mkubwa  yaani Ambassador Plenipotentiary, wapo watakaokuwa mabalozi wasio wa kawaida na  wenye nguvu zote na uwezo mkubwa yaani Ambassadors Extraordinary and Plenipotentiary na wapo watakaokuwa na Multiple Accreditation (Uwakilishi katika nchi zaidi ya Moja) na wale watakaokuwa na majukumu mengi zaidi (Multilateral Mission) kutokana na vituo au nchi watakazopelekwa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali.

Ni matumaini yangu tumeelewa. 

Itaendelea sehemu ya pili.

Wenu:

Abbas Mwalimu (Facebook|Instagram|Twitter)

+255 719 258 484

Uwanja wa Diplomasia (Facebook|WhatsApp)

Post a Comment

0 Comments