Wafanyakazi watatu wasimamishwa kazi Uhamiaji kwa kutumia nguvu

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Idara ya Uhamiaji imewasimamisha kazi wafanyakazi wake watatu kutokana na tukio la askari wa Uhamiaji kutumia nguvu dhidi ya Alex Raphael Kyai kama video fupi ilivyoonekana katika mitandao ya kijamii.
Akizungumza na wandishi wa habari leo Mei 30, 2021 Kamishina Jenerali wa Uhamiaji, Dkt Anna Makakala amesema Mei 27, mwaka 2021, Idara ya Uhamiaji ilimkamata mtuhumiwa wa utapeli anayefahamika kwa jina Alex Raphael Kyai katika Ofisi ya Uhamiaji Kurasini, Dar es salaam ambaye aliongozana na mteja wa huduma za pasipoti, aliyemtambulisha kama mkewe.

Aidha, Dkt.Makakala amesema baada ya mahojiano, ilibainika kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa na tabia ya kuwalaghai na kupokea fedha kutoka kwa wateja mbalimbali ili waweze kupata pasipoti kwa haraka, pia mtuhumiwa huyo amekuwa akijitambulisha kama Mtumishi wa Taasisi nyeti ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

"Idara ya Uhamiaji inakiri kutokea kwa tukio hilo na pia inalaani kitendo kilichofanywa na askari wa Uhamiaji kwa kutumia nguvu kinyume cha sheria na maadili ya kazi zao, hata hivyo Idara ya Uhamiaji tayari imechukua hatua za kinidhamu dhidi ya askari hao," amesema Dkt.Makakala.

Idara ya Uhamiaji inatoa wito kwa wananchi wote wanaohitaji huduma za kiuhamiaji kufika wenyewe katika ofisi za Uhamiaji, pia Uhamiaji wanawahakikishia kwamba idara itaendelea kutoa huduma zake kwa weled, uwazi na bila kutumia mtu wa kati ( Vishoka) Na Idara hiyo ya Uhamiaji inaomba kupata ushirikiano kutoka kwa wananchi kwa kutoa taarifa za watu wanaofanya vitendo vya aina hiyo.

Aidha, Idara ya Uhamiaji imetoa onyo kwa yeyote ambaye atajaribu kujifanya kuwa Afisa wa Uhamiaji au Afisa wa Serikali ili kumsaidia mtu mwingine kwa maslahi yake binafsi hatua kali dhidi yake zitachukuliwa kwa mujibu wa Sheria.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news