Wanafunzi 7,400 kushiriki mashindano ya Umitashumta na Umisseta

Na Asila Twaha, OR-TAMISEMI

Takriban wanafunzi 7,400 wanatarajiwa kushiriki Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA yatakayofanyika mkoani Mtwara.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe amesema jumla ya washiriki 3,600 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara wanatarajiwa kushiriki mashindano ya UMITASHUMTA na washiriki 3,800 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar watashiriki katika Michezo ya UMISSETA.

"Ufunguzi wa mashindano hayo utafanyika tarehe 08/06/2021 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona uliopo katika Manispaa ya Mtwara ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa," amesema.

Aidha, amesema mashindano ya UMITASHUMTA yatafanyika kuanzia Juni 6 mpaka Juni 19, 2021 ambapo michezo ya UMISSETA itaanza Juni 19 hadi Julai 3, 2021.

Prof. Shemdoe ameitaja michezo itakayoshindaniwa kwa upande wa UMITASHUMTA ni pamoja na mpira wa miguu kwa wasichana na wavulana, mpira wa miguu maalum kwa wavulana wenye ulemavu wa kusikia, na netiboli.

Michezo mengine ni mpira wa goli kwa wasichana na wavulana wasioona na wenye uoni hafifu, mpira wa wavu kwa wasichana na wavulana, na mpira wa mikono kwa wasichana na wavulana.

Mengine ni mpira wa meza kwa wasichana na wavulana, riadha jumuishi, kwaya na ngoma.

Aidha, amesema awamu zote mbili zitahusisha mashindano ya usafi katika mazingira wanayoishi kwa ujumla wake pamoja na nidhamu yao wakiwa kambini na michezoni.

"Niwaalike Watanzania wote kuja Mtwara kushuhudia vijana wetu wakionesha vipaji nabvipawa vyao katika michezo na sanaa," amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news