Watatu mahakamani kwa makosa 119 ikiwemo udanganyifu

Watu watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kwa makosa 119 ikiwemo kosa la kufanya udanganyifu, kughushi nyaraka, kutumia nyaraka za uongo ili kujipatia fedha kiasi cha Shilingi milioni 309.96, mali ya taasisi ya kifedha ya Letshego Tanzania Limited maarufu kama FAIDIKA.
Akisoma mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Pamela Mazengo, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Lucy Kyusa amesema washitakiwa hao wanadaiwa kufanya makosa hayo katika kipindi cha mwaka 2014 hadi 2017 katika wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Kyusa amewataja washitakiwa hao kuwa ni John Lyasenga ambaye alikuwa meneja wa FAIDIKA, Beatrice Mbwambo aliyekuwa afisa mikopo na Justine Mwimo aliyekuwa afisa wa Benki ya NMB.

Aidha, Kyusa amesema washitakiwa hao kwa nyakati tofauti walifanya udanganyifu, kughushi nyaraka kwenda kwa mkurugenzi wa wilaya ya Same wakiomba watumishi mbalimbali wa wilaya hiyo wasikatwe makato huku wakijua kufanya hivyo ni kosa.

Mazengo ameahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu atakapofika mshitakiwa wa pili, Mbwambo, ili wasomewe mashitaka yote kwa pamoja na kupangiwa tarehe ya kusikilizwa kwa kesi hiyo.

Hakimu Mazengo amesema dhamana za washtakiwa hao ziko wazi iwapo watatimiza masharti ya dhamana hiyo kwa mujibu wa makosa waliyoshitakiwa.

Post a Comment

0 Comments