Benki ya AfDB yamuahidi Rais Samia neema kwa Watanzania

Na Mwandishi Diramakini

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB Dkt. Adesina Akinumwi, amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwa benki hiyo itaendelea kufadhili miradi ya maendeleo hapa nchini na ipo tayari kufadhili miradi mipya kwa kuwa Tanzania ina sifa za kuendelea kupata ufadhili.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza kwa njia ya simu masuala mbalimbali ya Kimaendeleo na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dk. Adesina Akinwumi, ambaye alikuwa akizungumza kutokea Makao Makuu ya Benki hiyo Abidjan nchini Ivory Coast Juni 11, 2021.

Dkt. Adesina amesema hayo Juni 11, 2021 akiwa mjini Abdjan nchini Ivory Coast, wakati akizungumza kwa njia simu na Rais Samia akiwa Ikulu, Jijini Dar es Salaam, kuhusu uhusiano wa Tanzania na Benki hiyo ambayo imekuwa ikifadhili miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini

Katika mazungumzo hayo Dk. Adesina alianza kwa kutoa pole kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dk. John Magufuli na kumpongeza Rais Samia kwa kupokea kijiti cha Urais.

Dkt.Adesina amesema, Tanzania inafanya vizuri katika uchumi na ana matumaini makubwa kuwa Rais Samia ataendeleza jitihada zilizokuwa zikifanywa na mtangulizi wake.

Pia Dkt. Adesina ameahidi kuwa, AfDB itatoa ufadhili kwa Tanzania ili kuanzisha Benki za Wajasiriamali zitakazowakopesha vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi stadi pamoja na kujihusisha na kilimo, jambo litakalosaidia kupungua kwa tatizo la ajira kwa vijana na kuwaongezea kipato.

Aidha, Dkt. Adesina amemualika Rais Samia kuhudhuria mkutano wa uwekezaji utakaowaleta wawekezaji wakubwa pamoja ambao unatarajiwa kuvutia mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuwekeza katika nchi mbalimbali. 

Rais huyo amesema, AfDB imetenga Dola Bilioni 5 za Marekani kwa ajili ya kusaidia wanawake na ameomba Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa uwezeshaji wanawake kiuchumi ambapo Rais Samia amekubali ombi hilo", amesema Haniu katika Taarifa hiyo.

Dkt. Adesina ameahidi kuleta wataalamu wa benki hiyo hapa nchini ili wakutane na wataalamu wa Tanzania kwa ajili ya kupitia miradi ambayo tayari inafadhiliwa na benki hiyo na kujadili fursa za kuanzisha miradi mipya.

Kwa upande wake Rais Samia amemshukuru Dkt. Adesina kwa salamu zake za pole na pongezi na amemshukuru kwa benki hiyo kufadhili miradi mingi ya maendeleo hapa nchini ikiwemo inayotekelezwa chini ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa awamu ya pili na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na benki hiyo.

Rais Samia ameelezea kufurahishwa kwake na mradi wa AfDB wa kufadhili vijana wanaojihusisha na kilimo na wanaomaliza mafunzo katika vyuo vya ufundi stadi kwa kuwa ufadhili huo utawawezesha vijana wengi wa Tanzania kuzalisha mali.

Hata hivyo, pamoja na kumpongeza Dkt. Adesina kwa ushindi wake wa kuchaguliwa kuwa Rais wa AfDB kwa kipindi cha pili, Rais Samia amemuomba kuongeza nafasi za Watanzania wanaoajiriwa katika benki hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news