Bohari ya Dawa Tanzania kujenga kiwanda cha Kimataifa cha dawa Zanzibar, Rais Dkt.Mwinyi anena

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaunga mkono azma ya Bohari ya Dawa (MSD) ya kutaka kujenga kiwanda cha dawa hapa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Tanzania Meja Jeneral Saali Mhidze alipofika Ikulu kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Rais Dkt. Mwinyi ametoa pongezi hizo leo Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Meja Jenerali Saali Mhidze Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) akiwa amefuatana na ujumbe wake.

Katika maelezo yake Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kwamba, azma ya Bohari ya Dawa (MSD) ya kuja kuwekeza viwanda vya dawa hapa Zanzibar itasaidia kwa kiasi kikubwa hasa katika wakati huu wa janga la COVID -19 ambapo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kutoka nje sio mzuri.

Rais Dkt. Mwinyi ametoa pongezi kwa hatua zilizoanza kuchukuliwa na MSD za kutaka kuanzisha viwanda hapa Zanzibar ambazo zitapelekea kutotegemea sana dawa kutoka nje ya nchi hali ambayo athari yake imeweza kuonekana hasa katika kipindi hichi cha maradhi ya COVID -19 duniani.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa, hatua hiyo ya kuanzisha viwanda inaungwa mkono na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba tayari imeshatenga maeneo maalum ya viwanda na Serikali iko tayari kutoa ushirikiano wake.

Rais Dkt. Mwinyi ameeleza ipo haja ya kuonekana kwamba bidhaa zinazozalishwa Zanzibar nazo ni sehemu ya biashara kutoka Tanzania na kuondoa vikwazo vya kibiashara ambavyo hapo siku za nyuma vilikuwepo na kusababaisha biashara kati ya sehemu mbili za Muungano kuwa ngumu.

Pia, ameeleza azma ya Zanzibar ya kufanya bidhaa zozote zinazozalishwa hapa nchini kuagizwa nje ya nchi huku akieleza jinsi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inavyoiungana na Bohari ya Dawa (MSD) ya kuanzisha viwanda vya ndani hapa hapa nchini.

Amesema kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa ushirikiano mkubwa kwa Bohari ya Dawa (MSD), ili kuhakikisha azma yao hiyo inapatiwa ufumbuzi wa haraka hasa ikitambua kwamba ina uwezo na uzoefu mkubwa katika fani hiyo.

Rais Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuwa na viwanda vya aina mbalimbali lakini soko lake ni dogo ikilinganishwa na soko la Tanzania Bara na soko la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kueleza haja kwa Bohari ya Dawa (MSD) kueleza taratibu zinazohitajika ili kuondoa usumbufu kwa biadhaa zinazotoka Zanzibar.

Amesema kuwa, ni vyema Bohari ya Dawa (MSD) ikatoa maelekezo mazuri ili kuepuka kufanyika uzalishaji wa bidhaa kutoka Zanzibar na baadae kupata usumbufu wa soko la nje ya Zanzibar.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza haja ya MSD kuleta vijana ili kutoa utaalamu na mafunzo kwa watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kujifunza juu ya mfumo wa ununuzi, uhifadhi, usambazaji dawa, vifaa na vifaa tiba.

Amesema kwamba, iwapo Zanzibar itapata utaalamu kutoka MSD mafanikio zaidi yatapatikana katika mfumo mzima wa utoaji wa huduma hiyo hasa ikizingatiwa kwamba utaalamu huo kwa Zanzibar haujawa wa kuridhisha zaidi. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza mgeni wake Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Tanzania  Meja Jeneral Saali Mhidze, alipofika Ikulu kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Mapema Meja Jenerali Saali Mhidze akitoa maelezo yake kwa Rais wa Zanzibar, amesema kuwa, MSD inadhamiria kuja kuwekeza Zanzibar kiwanda cha dawa ambacho kitakuwa kikubwa kwa Tanzania, ukanda wa Afrika Mashariki na hata nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Amesema kuwa, dhamira ya MSD ya kuja kujenga kiwanda cha dawa hapa Zanzibar inatokana na mahitaji ya dawa pamoja na vifaa tiba vyenginevyo hapa nchini hasa katika wakati kama huu wa uwepo wa maradhi ya COVID-19 ambapo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kutoka nje ya nchi ni mgumu.

Ameeleza kuwa, Bohari ya Dawa (MSD), imekuwa ikichukua hatua za makusudi za kuhakikisha inajenga viwanda kwa ajili ya utoaji wa vifaa hivyo na tayari kwa upande wa Tanzania Bara tayari wameshaanza ujenzi wa viwanda kama hivyo.

Amesema kuwa,MSD imekusudia kupanua upatikanaji wa dawa na vifaa tiba hapa nchini na tayari viwanda vinne vimeshakamilika kazi ambayo imeanza tokea mwezi wa kumi mwaka jana na kusema kwamba baada ya miezi mitatu uhaba wa dawa unaweza kupungua kwa kiasi kikubwa hapa nchini.

Aidha, amesema kuwa kuna haja kwa Serikali kushirikiana na sekta binafsi katika suala zima la ujenzi wa viwanda vya dawa sanjari na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.

Meja Jenerali Mhidze amrsisitiza kwamba hatua za ujenzi wa kiwanda cha dawa hapa Zanzibar pia, kutasaidia kuleta ushirikiano wa uzalishaji wa dawa katika viwanda kati ya vile watakavyojenga Tanzania Bara na vile vya Zanzibar.

Sambamba na hayo, Meja Jenerali Mhidze alimuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kwamba kufanikiwa kwa azma yao hiyo ya ujenzi wa kiwadna cha dawa hapa Zanzibar kutasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa dawa hapa hapa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news