CCM yatoa maelekezo sita kwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika utaratibu wake kimetoa maelekezo kwa Wizara ya Fedha na Mipango kuelekea uwasilishaji wa Bajeti yake ya mwaka wa fedha 2021/2022 kwa kuzingatia kuwa Wizara ya Fedha na Mipango ndio kitovu cha mipango yetu ya maendeleo na pia, ndio wizara inayohusika na uwezeshaji wa rasilimali fedha kwa wizara nyingine zote, imetakiwa kuzingatia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Mwaka 2020/2025 fungu la 18 ambapo inataja kuwa Uchumi wa Nchi yetu unakuwa wa kisasa, shirikishi, na shindani ambao kwa kweli ni Uchumi wa kukuza viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Ili kufikia malengo hayo, Chama kimeielekeza Serikali kupitia wizara ya Fedha na Mipango katika Bajeti hii, kutekeleza yafuatayo;

1. Kuimarisha Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Chama kimeielekeza Serikali kuiimarisha kwa kuiwezesha Ofisi ya Msajili wa Hazina, ili iweze kuyasimamia mashirika ya Umma yazalishe kwa faida na kutoa mchango kwa maendeleo ya Taifa. Mathalani mashirika kama Shirika la Reli TRC, Bandari TPA, Shirika la ndege ATCL, Shirika la maendeleo ya Petroli TPDC, TTCL na mengine Mengi.

2. Ukuzaji wa uchumi

Katika mwaka wa fedha 2020/2021, ukuaji wa uchumi umekuwa ni wa kusua sua kutokana na sababu mbalimbali za ndani na nje ya Nchi ikiwemo athari za ugonjwa wa Uviko 19. Hivyo Chama Kimeielekeza Serikali kuhakikisha inabuni mikakati na mbinu za ukuzaji wa uchumi ili kuhakikisha ukuaji wa uchuni nchini unakua kwa wastani angalau asilimia nane kwa mwaka, ikilinganishwa na sasa ambao ukuaji ni asilimia 4.8

3. Udhibiti wa mfumuko wa bei

Ili kuwa na uchumi tulivu, Chama kimeielekeza serikali kuhakikisha kwamba, mfumuko wa bei unadhibitiwa na usizidi tarakimu moja 1. Udhibiti huu wa mfumuko wa bei utasaidia kukuza biashara za nje, hivyo kutupatia na kuongeza fedha za kigeni nchini. Fedha za kigeni husaidia kununua Mafuta (Petroli, Dizeli n.k) malighafi za viwanda, vipuri, na bidhaa mbalimbali ambazo hatuzalishi nchini ama hazitoshelezi.

4. Kupunguza utegemezi wa kibajeti

Ili kupunguza utegemezi wa misaada na mikopo kutoka nje ambayo mara nyingi imekuwa haiaminiki na hailetwi kwa wakati ili kukamilisha utekelezaji wa bajeti, Chama kimeielekeza Serikali kujikita katika ukusanyaji wa Mapato ya ndani ili kutekeleza dhana na sera ya kujitegemea, hivyo ni lazima serikali ihakikishe

I. Inaibua vyanzo vipya vya mapato vya ndani

II. Inaongeza Idadi ya walipa kodi

III. Inakusanya kodi kwa mifumo ya kielektroniki ili kuziba mianya ya udanganyifu na upotevu wa mapato ya serikali.

5. Uhimilivu wa Deni la Taifa

Chama kimeielekeza Serikali kuwa, Deni la Taifa linapaswa kuendelea kuwa himilivu na endapo tutalazimika kukopa, mikopo hiyo iwe ni yenye tija kwa taifa na isiyo athiri uhimilivu wa deni.

6. Uimarishaji wa mifuko ya utaoji wa mikopo

Chama kimeielekeza serikali kuhakikisha kinaimarisha mifuko ya utaoji wa mikopo kwa wananchi. Uwezo wa kifedha wa mifuko hii utawezesha wadau wengi nchini kuweza kukopa na kuendeleza shughuli zao kiuchumi, ikiwemo Viwanda, Nishati na Kilimo na hivyo kuimarisha uchumi wa nchi na pato la mtu mmoja mmoja. Mfano mifuko kama, Mfuko wa kusaidia sekta binafsi ya kilimo, Mfuko wa kudhamini mikopo ya mauzo nje ya nchi, Benki ya maendeleo ya kilimo, Benki ya Maendeleo TIB ikiwezeshwa itasaidai kuwezesha shughuli mbalimbalin za kiuchumi.

Wizara hii ya fedha ndio wizara wezeshi kwa wizara zote na taasisi nyingine, fedha zinazopelekewa ndio huwezesha mipango ya serikali kwenye taasisi zake katika shughuli za kawaida na maendeleo. Hata hivyo, uzoefu unaoenesha kuwa, Bajeti inayoidhinishwa na Bunge katika wizara husika hutolewa si kwa wakati na pungufu kwa kiwango kisichokidhi utelekezaji wa mipango/miradi iliyokusudiwa na wizara, hivyo kuathiri utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama. Hivyo Chama kimeielekeza serikali kuhakikisha fedha zilizoidhinishwa katika bajeti kwa kila wizara, zipelekwe zote na kwa wakati ili kutokwamisha mipango ya maendeleo iliyowekwa.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Shaka Hamdu Shaka
Katibu wa Halmashauri kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi.
04 Juni 2021.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news