Harbinder Seth 'yupo huru'

Leo Juni 16,2021 Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP), Sylvester Mwakitalu amesema, mfanyabishara Herbinder Seth anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, amekubali na kukiri makosa na kulipa faini na leo kama atakamilisha utaratibu ataachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kwa mujibu wa Jamii Forum, wakati hapo jana mahakamani alitokea Seth peke yake je kila mmoja ana msimamo wake? Tusubiri leo baadae.


Serikali yaafiki maombi majadiliano na Seth

Awali upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mtendaji wa PAP, Harbinder Seth, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wamepitia barua iliyoandikwa na mshtakiwa huyo na kufikia makubaliano kwa kile alichokiomba. Seth aliandika barua hiyo Juni 10, kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), akiomba kukiri mashtaka yake na kupunguziwa adhabu.

Barua hiyo ilijadiliwa kwa siku mbili na upande wa mashtaka na ule wa utetezi na kisha kutolewa mrejesho.

Wakili wa Serikali Mkuu, Marterus Marandu akisaidiana na Ladslaus Komanya jana alitoa maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Wakili Marandu alitoa maelezo hayo wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya upande wa mashtaka kuwasilisha mrejesho wa kile walichozungumza kati yao na Seth kwa ajili ya kuimaliza kesi hiyo.

“Kesi imekuja kwa ajili ya kutoa mrejesho wa barua iliyoandikwa na mshtakiwa huyu (Seth), niseme barua tumeshazipitia kwa pamoja na tumefikia mahali pa kukubaliana kuhusu kile ambacho mshtakiwa alikuwa anakiomba na baada ya hapo, tumekubaliana kuendelea na shauri hili,” alidai wakili Marandu na kuongeza:

“Kwa muktadha huo, upande wa utetezi kama hawatakuwa na pingamizi, naomba shauri hili lije mahakamani hapa kesho ( Juni 16) kwa ajili ya usikilizwaji,” alidai Marandu.

Baada ya kueleza hayo, Wakili wa Seth, Melchisedeck Lutema alikubaliana na maelezo ya upande wa mashtaka na kueleza kuwa huo ndio ukweli na ndio msimamo wa pande zote mbili za majadiliano waliyofanya.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hadi Juni 16 itakapoitwa kwa ajili ya usikilizwaji au majadiliano ya kuimaliza kesi.

Hata hivyo, jana Seth alikuwepo mahakamani peke yake, wakati upande wa mashtaka walipowasilisha mrejesho huo.

Itakumbukwa Juni 10, Mahakama hiyo ilikubali upande wa mashtaka kufanya mazungumzo na mshtakiwa huyo ya kuimaliza kesi hiyo. Mahakama hiyo ilirihusu majadiliano hayo baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha ombi mahakamani hapo la kutaka kufanya majadiliano na Seth na kisha kutoa mrejesho wa kile walichozungumza kwa ajili ya kuimaliza kesi.

Mbali na Seth, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ambao hawajaandika barua ya kukiri mashtaka yao kwa DPP ni aliyekuwa Mwanasheria wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege na Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa kampuni ya IPTL, James Rugemalira.

Katika kesi ya msingi, Seth na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 12 likiwemo la kutakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.Uamuzi wa Mahakama soma hapa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news