Hatua kwa hatua aliyoyasema Rais Samia mbele ya Wahariri wa vyombo vya habari

NA GODFREY NNKO

Kwa mara ya kwanza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeteta na wahariri na wakuu wa vyombo vya habari nchini Tanzania.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema, kwa kipindi hiki ana mambo ya kushughulikia.

Pia amesema kuwa, anakwenda kufungua nchi na ili hilo liweze kufanyika ni lazima nchi iwe na amani.

Mheshimiwa Rais Samia ametoa mwelekeo wake huo pale alipoulizwa na waandishi wa habari ni lini ataruhusu mikutano ya kisiasa iwe rasmi.

Rais Samia amesema, kama alivyosema huko nyuma, atakaa na wanasiasa ili kuona wanakwendaje na siasa zetu hapa nchini.

"Sasa hivi kuna mambo mengi ya kushughulikia. Tuna mambo mengi tunataka kuyafanya nimesema ninakwenda kuifungua nchi,"amesema Rais Samia.

Rais Samia ametolea mfano kuhusiana na kuongezeka kwa wawekezaji nchini huku akifafanua kwamba Machi hadi Mei, mwaka huu wawekezaji waliokuja kuwekeza nchini ni mara mbili zaidi ya waliokuja mwaka jana katika kipindi kama hicho.

"Tunapofungua hivi wawekezaji wanakuja, uchumi unakuwa fedha zinajaa mifukoni, watu wanalipa kodi. Na hayo ili yafanikiwe inatakakiwa nchi iwe na amani, tukisema hii ni moja au sita, basi akija mwekezaji akute ni moja au sita kweli, kwa sababu uchumi ukipanda kila mmoja atafaidika.Na kwa kufanya hivyo, nchi lazima iwe imepoa, naomba nipeni muda tuite wawekezaji uchumi ufunguke, halafu tutashughuka mengine.

"Lakini sasa hivi mnaona mikutano ya ndani ya kisiasa inafanyika, kamati kuu za vyama zinafanya mikutano yake na wabunge wanaruhusiwa kufanya mikutano kwenye majimbo yao,"amesema.

Rais Samia akizungumzia suala la Katiba amesema ni la maana sana, lakini wapewe muda."Tupeni muda tuisimamishe Tanzania, tusimame tujenge nchi pamoja na nyie,"amesema.

Rais Samia alipoulizwa kuhusu ni mambo gani katika kazi ngumu ya Urais yanamtia moyo amesema ni pale anapoona yale ambayo ameyafanya ndani ya siku 100 yanaungwa mkono na mengi alikuwa hayajui kama ameyafanya.

Pia alipoulizwa kuhusu uteuzi wake ambao unaonekana kuwaacha wana CCM ambao walipigania chama wakati wa uchaguzi, Rais Samia amesema wanaochaguliwa kwenye uteuzi wake ni vijana wa Kitanzania, sio vijana kwa tafsiri wanayoijua.

Amesema, katika walioteuliwa kuna waliotoka upinzani, kuna walioko upinzani na wana CCM waliofanya kazi kubwa ya kukipigania chama.

"Kila sekta nimenyakua nyakua. Wazee kabisa tunawapumzisha, lakini vijana kama mimi na ninyi tunakwenda nao,"amesema Rais Samia.

Mheshimiwa Rais Samia alipoulizwa ni lini magazeti yaliyofungiwa na mengine yakiwa yamemaliza kutumikia dhabu zilizotolewa, lakini hadi sasa hayajafunguliwa amesema, anajua kuna magazeti yameshamaliza adhabu zao, hivyo wahusika waende kuomba leseni mpya.

"Hakuna sababu ya kuendelea kufungiwa. Lakini lazima sheria ziheshimiwe, tukosoeni, lakini tuoneshe na njia, tuzingatie heshima na adabu za Kiafrika," amesema Rais Samia.

Wakati huo huo akizungumzia kuhusu Ripoti ya Uchunguzi Maalum ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusiana na matumizi ya fedha zilizotumika kwa kipindi cha miaka mitatu, alioagiza wakati akiapisha makatibu wakuu, Rais Samia amesema, Jumatano anapokea ripoti hiyo na umma utajua kilichomo kwenye hiyo ripoti.

Pia alipoulizwa kuhusu tathmini yake tangu aingie madarakani ndani ya siku 100 na anaielezaje kazi ya urais, Rais Samia amesema.

"Ni ngumu, lakini kwa sababu urais ni taasisi na kuna vyombo kadhaa navyo vinasaidia, hivyo hapo ndipo unafuu ulipo,"amesema.

Mheshimiwa Rais amesema, anapopelekewa jambo kwa ajili ya maelekezo au kwa maamuzi, jambo hilo linakuwa limeishachakatwa, hivyo linakuwa na unafuu, lakini sio rahisi kihivyo, kwani lazima ajue kinachoendelea ndani ya nchi nzima.

"Kwa siku yanakuja mafaili zaidi ya 30 na inabidi usome na uelewe. Kazi ya urais inakuwa rahisi zaidi pale unapokuwa umejipanga na kujaza fomu kwamba unataka kuwania nafasi hiyo. Mimi nilikuwa nina bonge la kaka, lakini lilipokuja kwangu niwahakikishia kwamba naweza kwenda nalo, hii ni kazi yetu pamoja, kwa pamoja tutafika," amesema Rais Samia.

Amesema, siku 100 alizokaa madarakani hata yeye ameshangaa hata lile limefika. "Tumeweza kuhimili vishindo vya kutetereka uchumi wa dunia, uchumi bado imara, tuna akiba ya fedha za kigeni ya miezi sita mbele na kiasi hicho duniani kinakubalika na ni kati ya kigezo kilichotufikisha uchumi wa kati," amesema.

Pia amesema yote inakwenda vizuri na tutakwenda kwa jinsi tulivyojipanga. "Mpaka sasa hivi tunakwenda vizuri,"amesema.

Katika hatua nyingine Rais Samia ametoa takwimu za maambukizi ya wimbi la tatu la ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) nchini, ambapo nchini kuna wagonjwa zaidi ya 100, huku chini ya 70 wakiwa kwenye matibabu ya kutumia Oksijeni

"Kuna wagonjwa zaidi 100 kati yao 70 wapo kwenye matibabu ya gesi na wengine matibabu ya kawaida, sio wengi, lakini tujikinge wasiongezeke,"amesema.

Rais Samia amesema alipoingia madarakani alitamani ashughulikie janga hilo kama linavyoshughulikiwa na Dunia, hivyo alianza kuagiza hatua mbalimbali zinazoshauriwa na wataalam wa afya zianze kuchukuliwa.

Pia amesema, kuna jamii ya kimataifa wanaofanyakazi nchini ambapo walitaka chanjo iletwe ili watu wao waweze kuchanjwa. Rais Samia amesema, maamuzi ya Serikali ni kwenda kama duniani inavyokwenda.

Amesema, wakati wa wimbi la kwanza la ugonjwa wa Corona alikuwa na madhara kutokana na tahadhari zilizochukuliwa, lakini wimbi la pili lilikuwa na madhara kuliko wimbi la pili na sasa hawajui wimbi la tatu hali itakuwaje.

Rais Samia amesema, wagonjwa waliopo sio wengi, lakini alitoa wito kwa Watanzania kuchukua tahadhari ili wasiongezeke zaidi ya hapo.

"Tulisema twende kama ulimwengu unavyotaka, Tuchanje anayetaka chanjo, Watanzania wengi hasa wafanyabiashara wamepata chanjo, wameenda Dubai, Afrika Kusini na kwingine.Lakini tumesema jamii ya kimataifa walete chanjo zao ziletewe wachanjwe chini ya mamlaka zetu wakimaliza ndipo chanjo zao ziondoke,"amesema Rais Samia.

Amesema, wameharakisha kusema na Tanzania tupo kwenye mpango wa kupata chanjo ili nchi iweze kupata chanjo hizo. "Sasa ni chanjo gani ije, watatuambia wataalam wetu,"amesema.

Pia amesema wapo ambao wamejitolea kutupa msaada, hivyo hata wataalam wetu watasema ni chanjo gani ije huku akiwataka Watanzania kuchukua tahadhari na kama wanaona kufukiza nyungu au kutumia dawa gani, wafanye hivyo, lakini wao wanazosisitiza ni zile ambazo wataalam wanasema. (diramakini@gmail.com).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news