IAEA yaikatia tamaa Iran ukaguzi vinu vya nyuklia

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

IAEA ambalo ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti Matumizi ya Nishati ya Nyuklia lenye makao yake makuu mjini Vienna nchini Austria limesema ukaguzi wa muda katika vinu vya nyuklia vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unazidi kuwa mgumu.
Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi. (Picha na Leonhard Foeger/Reuters/Diramakini Blog).

Rafael Grossi ambaye ni Mkuu wa IAEA amesema kuwa, ugumu huo unatokana na Iran kutofafanua kuhusu maeneo yake ambayo haikuyataja awali yanayodhaniwa kuendesha shughuli za kurutubisha madini ya urani.

Grossi amebainisha kuwa,kukosekana kwa majibu kunaathiri uwezo wa shirika hilo kuelezea matarajio ya amani kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Grossi ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Vienna, Austria huku akibainisha kuwa, anaona uwezekano wa kufanyika ukaguzi wa muda wa vinu vya nyuklia umepungua.

Miezi mitatu iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilisitisha shughuli za ukaguzi za IAEA, hatua iliyolifanya shirika hilo kuanzisha makubaliano ya ukaguzi wa muda wa miezi mitatu ili kuiruhusu iendelee na shughuli zake, licha ya kupungua kwa kiwango cha uwezekano huo.

Mkuu huyo amesema kuwa,ana wasiwasi kwamba shughuli za kurutubisha madini ya urani zinaendelea kwenye maeneo matatu nchini Iran ambayo hayajatangazwa na kwamba maeneo hayo bado hayajulikani.

Grossi ambaye alikuwa akizungumza katika mkutano wa bodi ya magavana inayozihusisha nchi 35 na unaofanyika kila baada ya miezi minne alisema, duru kadhaa za mazungumzo kuhusu vinu hivyo hazikutoa ufafanuzi wowote ule.

''Matarajio yangu kuhusu mchakato huu hayakutimizwa. Ni wazi kabisa nilikuwa natarajia mchakato huu utaweza kuturuhusu kusonga mbele kufanya maendeleo ya wazi kuelekea kupata ufafanuzi wa masuala yote haya. Lakini hayajafanyika,''amefafanua Grossi.

Mbali na hilo, Mkurugenzi huyo wa shirika la IAEA alielezea wasiwasi kuhusu urutubishaji wa madini nchini Iran ambao umekuwa ukiendelea tangu mwezi Aprili.

Aidha, baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya kimataifa ya nyuklia mwaka 2018, Iran ilibadili mwelekeo kuhusu masharti iliyowekewa chini ya mkataba huo.

Hata hivyo, wanadiplomasia kutoka Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Urusi na China wamekuwa wakijaribu kuwa mpatanishi kati ya Marekani na Iran katika mazungumzo yanayoendelea mjini Vienna tangu mwezi Aprili. Lengo kuu likiwa ni kuyaokoa makubaliano ya nyuklia ya Iran.

Aidha, wanadiplomasia hao wanaamini kupitia mazungumzo yao ya kuyafufua makubaliano hayo ya mwaka 2015 yanayojulikana kama JCPOA, kabla ya uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika Juni 18, mwaka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news