MANYARA, ARUSHA ZANG’ARA FAINALI YA MITA 3000 UMISSETA

Na Mathew Kwembe, Mtwara

Wanariadha Damian Patrick wa Arusha na Loema Awaki kutoka Manyara wameshinda fainali za mbio za mita 3000 zilizofanyika leo katika uwanja wa chuo cha ualimu Mtwara.

Patrick ambaye ameonyesha uwezo mkubwa katika mashindano ya riadha ya mbio ndefu katika UMISSETA ya mwaka huu, alishika nafasi ya kwanza kwa wavulana na alitumia muda wa dakika 8:41:91, huku aliyemfuatia Benson Masawe wa Manyara akitumia muda wa dakika 8:57:10 na nafasi ya tatu ikishikwa na Robert Mayengo wa Geita ambaye alitumia dakika 8:57:38.
Baadhi ya wanariadha walioshiriki fainali za mbio za mita 3000 kutoka mikoa mbalimbali nchini wakichuana leo katika uwanja wa chuo cha ualimu Mtwara.


Kwa upande wa wanariadha wasichana, Awaki alishinda mbio hizo akikimbia kwa muda wa dakika 10:07:81, akifuatiwa na mwanariadha kutoka Mara, Neema Siruri ambaye alitumia muda wa dakika 10:15:22, huku nafasi ya tatu ikishikwa na mwanariadha Honoratha Benedicto wa Singida ambaye alitumia muda wa dakika 10:21:22.

Kufuatia kumalizika kwa fainali za mbio za mita 3000, mshindi wa kwanza kutoka kwa wavulana na wasichana atapewa medali ya dhahabu, mshindi wa pili, fedha na mshindi wa tatu atapata medali ya shaba.

Wakati huo huo michezo mingine ya UMISSETA imeingia katika hatua ya robo fainali ambayo inatarajiwa kuanza hapo kesho na tayari baadhi ya michezo timu zilizoingia hatua hiyo zimekwishajulikana.
Mshindi wa kwanza wa fainali za mbio za mita 3000 wavulana Damian Patrick (17)ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili kutoka shule ya kimataifa ya St Patrick iliyopo Sakina Arusha akimalizia mbio hizo leo asubuhi katika uwanja wa chuo cha ualimu Mtwara.


Kwa upande wa Volleyball timu zilizoingia hatua hiyo kwa wavulana ni Dar es salaam, Arusha, Mtwara, Tabora, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Unguja.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo kesho Dar e salaam itacheza dhidi ya Kigoma, Mbeya itachuana na Arusha, wenyeji Mtwara wamepangwa kucheza na Unguja na Mwanza watacheza na Tabora.


Kwa upande wa Volleyball wasichana timu zilizofanikiwa kuingia robo fainali ni Mtwara, Tabora, Mbeya, Simiyu, Dar es salaam, Tanga, Mara, na Manyara.
Mshindi wa kwanza wa fainali za mbio za mita 3000 wasichana Loema Awaki (18)ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu kutoka shule ya Sekondari ya Gunyoda wilayani Mbulu mkoani Manyara mara baada ya kumaliza mbio za mita 3000 leo asubuhi katika uwanja wa chuo cha ualimu Mtwara.

Katika hatua hiyo Mtwara itacheza dhidi ya Tanga, Dar es salaam itacheza na Tabora, Mbeya imepangwa kuchuana na Manyara na Mara atacheza na Simiyu.

Katika mchezo wa mpira wa mikono, timu zilizoingia robo fainali kwa wavulana ni Tabora, Morogoro, Unguja, Dar es salaam, Tanga, Rukwa, Arusha na Geita.

Mpira wa mikono wasichana, timu zilizoingia hatua hiyo ni Morogoro, Geita, Songwe, Tabora, Mbeya, Dar es salaam, Unguja na Tanga.

Post a Comment

0 Comments