Mganga Mkuu wa Serikali afanya ziara Hospitali ya Rufaa ya Amana

Na Mwandishi WAMJW 

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt.Aifelo Sichalwe amefanya ziara fupi katika hospitali ya rufaa ya Mkoa Amana Jijini Dar es Salaam yenye lengo la kukagua Utekelezaji wa maagizo ya Viongozi wa Wizara waliyoyatoa kwa nyakati tofauti kuhusu maandalizi na utayari wa Watumishi wa afya katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Covid-19. Dkt.Aifelo Sichalwe Mganga Mkuu wa Serikali akiongea na watumishi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa,Dkt.Sichalwe ameridhishwa na utayari wa Hospitali hiyo wa kukabiliana na Magonjwa ya mlipuko ikiwemo Corona.

Akiwa hospitalini hapo Dkt. Sichalwe amezungumza na uongozi wa hospitali hiyo ambapo amewataka viongozi hao wa wafanyakazi kujitayarisha kwa vifaa na matibabu kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Amesema Kama watumishi wa Afya, ni vyema kuwa tayari wakati wowote hususan katika kipindi hiki ambacho nchi jirani wamekumbwa na wimbi la tatu la ugonjwa wa Corona kwa kuwa raia wa nchi hizi wana muingiliano mkubwa wa shughuli za kiuchumi na biashara, hivyo kama nchi hatuna budi kujipanga.
Mitambo ya kufua hewa ya Oksjeni iliyosimikwa Kwenye hospitali ya Rufaa ya mkoa.

Sambamba na kikao hicho Dkt.Sichalwe amekagua miundombinu ya hospitali na utekelezaji wa afua za kuzuia maambukizi mahali pa kazi (Infection, prevention and control). 

Ameupongeza uongozi wa hospitali hiyo kwa juhudi na jitihada kubwa wanayofanya hospitalini hapo kwa lengo la kuzuia ueneaji wa maambukizi kwani watumishi wote walikutwa wamevaa barakoa na sehemu za kunawia zenye sabuni na maji zikiwepo kila wodi, sehemu ya mapumziko na getini.

“Nimeona mmevaa barakoa, mnatoa elimu kwa wananchi pia. Haya mnayotekeleza hapa ni kama darasa kwa wananchi wote wanaokuja kupata huduma hapa nao watakuwa mabalozi kwa wenzao kwenye jamii. Nina imani utekelezaji huu mnaendeleza hata baada ya kazi”.

Aidha, Dkt.Sichalwe amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa nchini kusimamia utekelezaji wa afua hii, kwani unatukinga siyo tu na ugonjwa wa covid 19 bali na Magonjwa mengine mengi yanayosababishwa na kula vitu kwa mikono isiyo safi na kuvuta hewa yenye vimelea vya maambukizi.
Dkt.Sichalwe akiangalia moja ya mashine zilizopo kwenye wodi zilizopo hospitalini hapo Mganga Mkuu wa Serikali akiongea na baadhi ya viongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana

Vilevile Dkt.Sichalwe ametembelea mtambo maalumu wa kuzalisha hewa ya Oksijeni hospitalini hapo ambapo ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza zaidi ya Milioni 600 ili kuhakikisha wanaokoa Maisha ya watanzania wanaohitaji huduma hiyo.Mtambo huo wenye matoleo Zaidi ya 89, unauwezo wa kuzalisha mitungi 200 ya hewa ya Oksjeni kwa masaa 24 na hospitali ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa wenye uhitaji 150 kwa wakati mmoja.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume amesema kuwa juhudi hizo zinaendelea kufanywa na hospitali zote ndani ya Dar es Salaam ili kuhakikisha wanalidhibiti ipasavyo wimbi hili la tatu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news