NEC ya CCM yampongeza Rais Samia kwa kuivusha Tanzania salama

Na Doreen Aloyce, Diramakini Blog

HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM ya Taifa (NEC) imekutana leo jijini Dodoma katika kikao cha kwanza na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuivusha nchi salama katika kipindi cha mpito baada ya kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli huku Taifa likibaki kuwa na amani na utulivu.
Akizungumza leo Juni 29 na waandishi wa habari Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka amesema, kikao hicho kimeazimia pongezi hizo wampe kwa maandishi kwa kumpongeza kwa kupokea madaraka katika kipindi kigumu.

"Wajumbe wa Halmashauri Kuu wameona anaenda vizuri katika uongozi wake kwa kuongoza kwa uadilifu na haki kwa kusimamia misingi ya kidemokrasia,"amesema Shaka.

Aidha, amesema katika azimio lingine la kikao hicho wajumbe wameona Serikali yake imeendelea kuwajali wananchi wa chini hasa katika bajeti iliyowasilishwa ya 2021/22 kwani imetoa dira inayoonesha Serikali inakwenda kupambana na umasikini kwa vitendo.

Katika hatua nyingine Halmashauri Kuu imempongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt.Hussein Ally Mwinyi kwa kusimamia vyema Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM) huko Visiwani Zanzibar.

"Kwa upande wa kiuchumi wa blue umeonekana wawekezaji wameendelea kujitokeza huku Amani na utulivu ikizidi kuimarika,"amesema Shaka.

Shaka amesema, Rais Samia katika kikao hicho amewasisitiza wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kwamba bado wanajukumu kubwa la kwenda kusimamia Ilani huku akiwataka kusimamia miradi yote ambayo inatekelezwa na Serikali ili imalizike haraka na kwa wakati.

Pia amewataka kupokea maelekezo na wasiwe na uoga wala hofu bila kusita kusema kama miradi hiyo haitekelezwi ipasavyo hivyo kuhakikisha miradi iliyoanzishwa itatekelezwa kwa wakati na ufanisi.

Kikao hicho cha NEC kilikuwa ni kikao cha kawaida kwa mujibu wa katiba ya chama ambacho ufanyika kila baada ya miezi sita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news