Sabaya, walinzi wake wapelekwa Gereza la Kisongo kwa tuhuma sita

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Lengai Ole Sabaya (34) na walinzi wake wamepelekwa Mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo lililopo nje kidogo ya Jiji la Arusha kwa tuhuma za kutenda makosa mbalimbali ambayo hayana dhamana.
Hayo yamejiri leo Juni 4, 2021 baada ya Sabaya ambaye alikuwa mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro na walinzi wake watano kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha.

Watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa mbalimbali likiwemo la uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kupokea rushwa.
Hatua hiyo inakuja zikiwa zimepita siku chache baada ya Lengai Ole Sabaya kusimamishwa kazi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Mei 13, 2021 ili kupisha uchunguzi kwa tuhuma ambazo zinamkabili.

Sabaya amefikishwa mahakamani hapa mchana akiwa amefungwa pingu na baada ya wote kushuka kwenye magari ya polisi walitakiwa kuchuchumaa na kisha kupelekwa katika chumba maalum na baadaye kuingizwa mahakamani ili kuruhusu taratibu zingine ziendelee.
MWANDISHI DIRAMAKINI amebainisha kuwa, waendesha mashtaka wa Serikali, Tumaini Kweka, Abdallah Chaula na Tresla Garvas mbele ya Hakimu Mfawidhi, Martha Mahumbuga na Hakimu Mkazi Mkuu, Salome Mshasha wamesema Lengai Ole Sabaya na wenzake walitenda makosa hayo Januari 20 na Februari 9, mwaka huu wa 2021.Zinazomuhusu Lengai Ole Sabaya soma hapa pia.

Aidha, Kweka amesema, Lengai Ole Sabaya na wenzake watano anatuhumiwa kwa makosa ya kuunda genge la uhalifu, uhujumu uchumi, kujipatia fedha kwa njia ya rushwa na utakatishaji fedha ambapo Sabaya alijipatia shilingi milioni 90 kutoka kwa mfanyabiashara, Francis Mroso mkazi wa kwa Mromboo ambaye alikuwa anatuhumiwa kwa makosa ya ukwepaji kodi ili amsaidie jambo ambalo ni makosa.
Sabaya na walinzi wake wawili, Sylivester Nyengu (26) maarufu kicheche na Daniel Mbura (38) pia wanakabiliwa na makosa mawili ya ujambazi wa kutumia silaha wakidaiwa kuyatenda Februari 9, 2021.

Watuhumiwa hao wanadaiwa walimfunga pingu na kumpiga Bakari Msangi ambaye ni Diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Sombetini na kumuibia shilingi 390,000.

Aidha, huko eneo la Bondeni jijini Arusha wakitumia silaha, Lengai Ole Sabaya na walinzi hao wanatuhumiwa kumpiga, kumtishia silaha na kumpora Ramadhani Ayoub simu na shilingi 35,000, kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Juni 18, mwaka huu mahakamani hapo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news