TANESCO YAENDELEA KUIMARISHA MFUMO WA LUKU

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka leo Juni 29, 2021 akizungumza na vyombo vya habari katika Ofisi za TANESCO Mikocheni jijini Dar es Salaam amesema kuwa, kazi ya kuimarisha mfumo wa kuuza umeme wa malipo ya kabla (LUKU) bado inaendelea na maboresho ili kuimarisha zaidi uwezo wa mfumo huo kwa kuuongeza mfumo mbadala (backup).
Dkt. Mwinuka ameyasema hayo alipokutana na waandishi wa habari kutolea ufafanuzi jinsi TANESCO inavyojipanga kuondokana na changamoto ya kukosekana kwa mfumo wa manunuzi ya umeme pamoja na ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme nchini.

Aidha, Dkt. Mwinuka ameongeza kuwa, mfumo huo wa LUKU ulianza kufanya kazi Mei 19, 2021 mchana baada ya kutokea kwa hitlafu ya manunuzi ya umeme Mei 17 na 18, 2021 na hivi sasa kazi ya kujenga mfumo mbadala inaendelea.

"Hivi sasa tunaendelea na kazi ya kuhamisha taarifa kutoka kwenye mfumo wa msingi kupeleka kwenye mfumo mbadala baada ya kuukamilisha kuujenga," amesema Dkt. Mwinuka.

Ameongeza kuwa, katika kipindi hiki cha maboresho ya mfumo kutakuwa na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika manunuzi ya umeme kutokana na majaribio katika mfumo mbadala.

Amesema, iwapo wananchi wanapata changamoto ya kununua umeme kupitia mtandao mmoja, ni vyema kutumia mtandao mwingine pamoja na huduma za kibenki.

Post a Comment

0 Comments