'Tumieni Skuli ya Turkish Maarif Zanzibar kuwapa elimu watoto'

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi wa Zanzibar kutumia vyema fursa ya kuwepo Skuli ya ‘Turkish Maarif Zanzibar’ kwa kuwapeleka watoto wao ili kupata elimu.

Dkt. Mwinyi ametoa wito huo katika Ufunguzi na Mahafali ya Kwanza ya Kidato cha Sita ya Skuli ya ‘Turkish Maarif Zanzibar’ iliyopo Mombasa jijini Zanzibar.

Akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi; Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi amesema, kuwepo kwa Skuli hiyo kunaendana na malengo ya Serikali ya kupanua haki ya elimu nchini, hivyo akawataka wananchi kutumia vyema fursa ya kuwepo kwake na kupeleka watoto wao kusoma.Alisema uwepo wa skuli hiyo ni kigezo cha hatua ya maendeleo ya Elimu Zanzibar, pamoja na kuunga mkono malengo ya Serikali na hivyo akipongeza Uturuki kwa kufungua skuli hiyo.
Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mariam Mwinyi na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe.Simai Mohamed Said (katikati) wakifuatana na viongozi wengine alipowasili katika sherehe za ufunguzi wa Skuli ya Turkish Maarif Zanzibar iliyopo Kijiji cha SoS Mombasa jijini Zanzibar sambamba na mahafali ya kwanza ya kidato cha sita Skulini hapo ambapo amemuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi katika sherehe hiyo (kulia) ni Mjumbe wa Bodi ya Maarif kutoka nchini Uturuki, Prof.Aysen Gurshan na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Dkt.Mehment Gulluoglu.

Aidha, aliwapongeza wanafunzi wote waliomaliza masomo yao ya kidato cha sita kwa kufanikiwa vyema hususan wale waliopata alama za daraja la juu na kusisitiza umuhimu wa kudumisha nidhamu katika kufikia mafanikio.

Amesema, nidhamu pamoja na bidii ndio msingi wa kila kitu ikiwemo masomo, hivyo akasisitiza muhimu wa wanafunzi kuhudhuria skuli kikamilifu pamoja na kupenda masomo yao.

“Niwasihi watoto wanaomaliza kidato cha sita leo hii watafurahi, ila wajue hii ni hatua moja huko waendako vyuo vikuu watahitajika kuendelea na nidhamu zaidi, maana watapaswa kujisimamia wao wenyewe,”amesema.

Vile vile amewataka kuongeza bidii ili waweze kufanikiwa zaidi katika masomo yao ngazi za juu.

Katika hatua nyingine, amewataka wazazi na walezi kusimamia kikamilifu maendeleo ya elimu ya watoto wao,sambamba na wanafunzi kuepuka yale yote yatakayodumaza masomo yao, huku akiahidi Serikali kuendelea kulinda haki zao.

Aidha, alipongeza juhudi za wazazi na walezi katika kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya udhalilishaji pamoja na kushirikiana na serikali kupiga vita vitendo hivyo na kusisitiza umuhimu wa kuondokana na muhali.

“Tuwafundishe watoto wetu jinsi ya kujilinda dhidi ya udhalilishaji na kutoa taarifa pamoja na kuchukua hatua. Zanzibar bila ya udhalilishaji inawezekana,”amesema.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Simai Mohamed Said alisema, wizara hiyo imejipanga kufanya mageuzi mkubwa katika elimu ya msingi nchini, kwa kuanzisha mitaala ya kujenga umahiri ndani ya kipindi cha miaka mitano, ikiwa ni hatua ya kuwajengea msingi bora wa elimu.

Aliwataka walimu kuwasaidia wanafunzi wa elimu ya msingi ili waweze kujiamini pale watakapofikia elimu ya ngazi za juu.

Mapema, Mwalimu Mkuu wa Turkish Maarif Zanzibar, Ahmeid Ali Makame alisema, jumla ya wnaafunzi 49 walijisajili kufanya mitihani ya kidato cha sita mwaka 2021 katika masomo ya Sayansi na Sanaa na kufanikiwa kuwa miongoni mwa skuli bora kwa kupasisha wanafunzi 14 wa daraja la kwanza.

Aidha, katika risala yao, wanafunzi hao wamewashukuru walimu wao kwa kubeba dhima na kufanya juhudi kubwa zilizowezesha kufikia mafanikio, sambamba na wazazi kwa kuwasimamia vyema katika masomo yao.

Vile vile walitoa shukurani kwa Serikali kwa kuendelea kuiunga mkono skuli yao pamoja na juhudi za kuendeleza elimu nchini.

Katika hafla hiyo viongozi mbalimbali wa Kitaifa walishiriki, ambapo Mama Mariam Mwinyi alipata fursa ya kukata utepe pamoja na kutembelea madarasa mbali mbali kuangalia shughuli za kitaaluma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news