Wabunge wastaafu wa CHADEMA wafungua kesi ya Kikatiba dhidi ya Kamishna wa Magereza, Mwanasheria Mkuu

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mchungaji Peter Msigwa ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini mkoani Iringa na aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini mkoani Mbeya, Joseph Mbilinyi maarufu kama Mr.Sugu wamefungua kesi ya kikatiba dhidi ya Kamishna wa Magereza Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Uamuzi huo wameufikia wakipinga kile ambacho wanadai ni kukiukwa kwa haki zao za msingi na kikatiba wakati wanatumikia adhabu walizopewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya jijini Mbeya.

Wakili Charles Tumaini akizungumza leo Juni 2,2021 mkoani Dar es Salaam amesema, kesi hiyo namba 13 ya mwaka 2021 wameifunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Kuu ya Dar es Salaam.
Tumaini amesema kuwa, Juni 15,2021 kesi hiyo inatarajiwa kutajwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, ikiwa chini ya jopo la majaji watatu na mawakili wa upande wa utetezi zaidi ya 15.

Wakili huyo amewataja majaji hao kuwa ni Jaji Elinaza Luvanda, Jaji Angaza Mwaipopo pamoja na Jaji Edwin Kakolaki huku baadhi ya mawakili wa upande wa Utetezi ni Mpale Mpoki, Charles Tumaini, Barnabas Kaniki pamoja na Simon Patrick. 

Amesema,katika kesi hiyo madai yapo mengi, lakini yamewekwa katika sehemu tatu ambapo ni kulalamikia sheria za Magereza ambazo amedai zimepitwa na wakati.

Pia utamadumi wa namna ambavyo Jeshi la Magereza limekuwa likifanya kazi zao pamoja na sheria nyingine za nchi.

Amesema, lengo la kesi hiyo wanaamini kila mtu ni mfungwa mtarajiwa, hivyo wana jukumu la kuleta mabadiliko na mifumo ya sheria nchini.

Mchungaji Msigwa amesema wamefungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Kuu ya Dar es Salaam dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna wa Magereza Tanzania wakipinga kukiukwa kwa haki zao za msingi na za kikatiba wakati wakitumikia adhabu walizopewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya.

Amedai, yeye mwenyewe (Mheshimiwa Peter Msigwa) na viongozi wenzake walikuwa tunakabiliwa na kesi ya Jinai ya Mwaka 2019 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kukamilika kwa kesi hiyo Machi 10,2020 walipatikana na hatia na kutakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 40,000,000 au kutumikia kifungo cha miezi mitano jela. 

Ameongeza kuwa, "Hatukuweza kulipa kiasi hicho kwa wakati, kitu kilichopelekea kutumia kifungo jela mpaka pale kiasi hicho kilipopatikana ambapo tulilipa faini hiyo na kuachiwa huru,"amesema Mheshimiwa Msigwa.

Kwa upande wake,Mheshimiwa Mbilinyi yeye alikuwa anakabiliwa na kesi ya jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya ambapo alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita (6) bila faini ambapo yeye alitumikia kifungo mpaka alipopata msamaha wa jumla wa Rais Aprili 26, 2018.

"Kufungua kwa kesi hii ya kikatiba kunatokana na kukiukwa dhidi yetu kwa haki zetu za kikatiba na za msingi katika kipindi ambacho tulikuwa tunatumikia adhabu zetu.
"Kitendo cha mtu kupewa adhabu ya kutumikia kifungo gerezani hakina maana ya kuondoa utu wake aliopewa na Mwenyezi Mungu, kitu pekee anachotakiwa kukikosa ni uhuru wake na kuzuiliwa kwenda atakapo,haki zake zingine zote zilizoainishwa na sheria na mikataba ya kimataifa zinaendelea kuwepo na inabidi zilindwe na kuheshimiwa kama ambavyo mtu ambaye sio mfungwa anapata,"amebainisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news